Zarif: Ikiwa utaratibu uliowekwa na Ulaya hautotekelezeka, Iran itajitoa kwenye JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, ikiwa utaratibu maalumu ulioratibiwa na Ulaya kwa ajili ya kuyalinda makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hautakuwa na ufanisi wa utekelezaji, Iran itajitoa kwenye makubaliano hayo.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mazungumzo na waandishi wa habari kwenye ofisi ya uwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa. Akizungumzia jinsi Iran ilivyoheshimu na kutekeleza kikamilifu makubaliano ya JCPOA, Dakta Zarif amesema: Ikiwa utaratibu maalumu ulioanzishwa na Umoja wa Ulaya hautotekelezeka, kuna uwezekano Iran itajitoa kwenye makubaliano hayo.
Kufuatia kujitoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, nchi za Ulaya zimeamua kuanzisha utaratibu maalumu wa kurahisisha miamala ya malipo ya fedha kwa ajili ya bidhaa za Iran zinazosafirishwa nje na zinazoingizwa nchini ili kuhamasisha wadau wa kiuchumi kuendeleza kisheria miamala yao ya kibiashara na Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa Iran imekusudia kutumia sarafu nyinginezo badala ya dola katika uuzaji mafuta na katika miamala ya kimataifa ili kukabiliana na vikwazo vya uuzaji mafuta ilivyowekewa na Marekani.
Akijibu suali kwamba, kujitoa Iran kwenye JCPOA kunaweza kufungua njia ya kushambuliwa kijeshi, Dakta Zarif amesema, kama Marekani ingekuwa na imani kwamba itafanikiwa kuishambulia kijeshi Iran ingekuwa imeshafanya hivyo.
Mnamo tarehe 8 Mei mwaka huu, rais wa Marekani Donald Trump alijichukulia uamuzi wa upande mmoja na kukiuka majukumu ambayo nchi yake ilipaswa kuyatekeleza katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa kutangaza kujitoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.
Baada ya kuchukua hatua hiyo, serikali ya Washington imeanzisha kampeni za kila upande za mashinikizo dhidi ya Iran huku ikitumia kila njia kuzishawishi nchi nyingine ziunge mkono vikwazo vyake vya upande mmoja dhidi ya taifa la Iran.../