Njama za kikundi cha Munafiqeen na uchochezi dhidi ya Iran
Kukamatwa mwanadiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Ubelgiji kwa tuhuma bandia za kushiriki kwake katika mpango wa kushambuliwa kikundi cha kigaidi cha Munafigeen katika mojawapo ya viunga vya Paris, mji mkuu wa Ufaransa, ni uchochezi mpya dhidi ya Iran.
Baada ya kutokuwa na natija mkutano wa kila mwaka wa kikundi hicho uliofanyika yapata miezi mitatu iliyopita katika kiunga hicho, kwa magaidi hao na waungaji mkono wao, njama mpya ilianza kupangwa dhidi ya Iran. Njama hiyo imeipelekea Ujerumani kumkamata mwanadiplomasia mmoja wa Iran na kumkabidhi kwa maafisa wa Ubelgiji na pia Ufaransa kuchukua uamuzi wa kufunga akaunti za Wizara ya Intelijensia ya Iran nchini humo. Njama hiyo ilianza kupangwa sambamba na kufanyika safari ya Rais Hassan Rouhani wa Iran katika nchi mbili za Ulaya za Uswisi na Asutria, jambo linalothibitisha wazi kwamba njama hiyo ililenga kuvuruga safari hiyo na hatimaye kuharibu uhusiano wa Iran na Ulaya. Safari hiyo ilifanyika katika mazingira ambayo, baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Iran mashuhuri kama JCPOA, imekuwa ikitoa madai bandia na yasiyo na msingi ili kujaribu kuitenga Iran. Wakati huohuo, Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba Iran inalaani kila aina ya mabavu na ugaidi sehemu yoyote ile duniani na kwamba iko tayari kushirikiana na pande zote kwa ajili ya kufichua njama za kishetani na operesheni za kikundi cha Munafiqeen.'

Ni wazi kwa watu wote kwamba, Munafiqeen ni kikundi cha kigaidi na kilicho dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na ambacho daima kimekuwa kikifanya juhudi za kuvuruga uhusiano wa kigeni wa Iran na nchi nyingine za dunia na hasa za Ulaya. Pamoja na hali hiyo, misimamo ya wazi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na suala zima la utumiaji mabavu na ugaidi haliachi shaka yoyote ya ulazima wa kukabiliana na magaidi hao. Ni nchi za Ulaya ndizo zinatakiwa kuthibitisha ni kwa kiwango gani zinafungamana na siasa zao zinazotangazwa hadharani eti za kupambana na ugaidi kwa sababu ni nchi hizohizo za Ulaya na hasa Ufaransa, ndizo zinawapa hifadhi na makazi magaidi wa kikundi hicho. Kufanyika mkutano wa kila mwaka wa kikundi hicho mwaka huu katika kiunga cha Paris na kutolewa hotuba za wageni wa kulipwa na vilevile kushiriki mkutano huo wanasiasa mashuhuri wa nchi za Magharibi akiwemo Rudy Giuliani, wakili wa Rais Donald Trump wa Marekani, ni dalili inayothibitisha wazi uungaji mkono wa nchi hizo kwa ugaidi ambao umepelekea kuuawa shahidi Wairani wapatao 17,000.

Daniel Silver, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins University nchini Marekani anasema kwamba kila mtu anayekijua vizuri kikundi hicho anafahamu vyema kwamba Munafiqeen ni kikundi cha kigaidi na wala hapasi kukiunga mkono. Mtaalamu huyo wa Marekani anaendelea kusema: Inaonekana kuwa vyombo vya kijeshi na vya kiusalama vya Marekani vinashirikiana na Munafiqeen, hivyo inapasa kujulikana wazi bajeti ya kikundi hicho inadhaminiwa na nani.'
Katika mazingira hayo juhudi zozote za kugeuza ukweli wa mambo na kuanza kutoa tuhuma bandia zisizo na msingi hazitakuwa na faida yoyote kwa uhusiano wa Iran na Ulaya. Viongozi wa Ulaya wanapasa kuwa waangalifu kuhusiana na suala hilo ili wasije wakatumbukia katika njama ambazo zimepangwa na maadui. Kuhusu hilo, Bahram Qassimi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema jana Jumatao kwamba balozi wa Ujerumani aliitwa hivi karibuni katika wizara hiyo ili kubainishiwa malalamiko ya Iran kuhusiana na hatua ya kukamatwa nwabadiplomasia wa Iran na kukabidhiwa kwa serikali ya Ubelgiji.

Alisema mwanadiplomasia huyo wa Iran anapasa kurejeshwa mara moja mjini Berlin, na kwamba suala hilo limetokana na njama ya maadui wanaopinga kuboreshwa uhusiano wa Iran na Ulaya ambapo alisisitiza kuwa ni kikundi cha Munafiqeen ndicho kimepanga njama hiyo.
Kwa kutilia maanani uungaji mkono wa utawala haramu wa Israel na Marekani kwa kikundi hicho, ni wazi kuwa pande mbili hizo zinafanya juhudi kubwa za kuharibu uhusiano wa Iran na nchi za Ulaya ambapo kuvunjwa kwa njama hizo kunahitajia kuwa macho viongozi wa nchi za Ulaya.