Uganda yaomba kushirikiana zaidi na Iran katika sekta ya kilimo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49079-uganda_yaomba_kushirikiana_zaidi_na_iran_katika_sekta_ya_kilimo
Waziri wa Kilimo wa Uganda Vincent Ssempijja amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa katika sekta ya kilimo, hivyo ametaka mashirika ya kilimo ya Iran yawekeze nchini humo na pande mbili kushirikiana zaidi katika miradi ya kilimo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 27, 2018 12:11 UTC
  • Uganda yaomba kushirikiana zaidi na Iran katika sekta ya kilimo

Waziri wa Kilimo wa Uganda Vincent Ssempijja amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa katika sekta ya kilimo, hivyo ametaka mashirika ya kilimo ya Iran yawekeze nchini humo na pande mbili kushirikiana zaidi katika miradi ya kilimo.

Ssempijja ametoa wito huo katika mazungumzo na balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uganda Sayyed Morteza Mortazavi. 

Waziri wa Kilimo wa Uganda ameashiria uwezo mkubwa wa mashirika ya Iran katika sekta ya kilimo na akakaribisha kuwepo kwao nchini Uganda na kushirikiana pamoja na kuwekeza katika sekta mbalimbali za kilimo nchini humo.

Vincent Ssempijja amesema, mashirika ya Iran yanaweza kushirikiana na yale ya Uganda katika kilimo cha pembejeo, uanzishaji mifumo mipya ya umwagiliaji, kuanzisha kituo cha kisasa cha wanyama wa mifugo, kujenga karakhana za bidhaa za mazao ya kilimo na vilevile kutoa mafunzo ya kitaalamu kuhusiana na ufungaji bidhaa, utafuatji masoko  na uzalishaji bidhaa za kilimo.

Balozi wa Iran nchini Uganda Sayyed Morteza Mortazavi (kushoto) na Waziri wa Kilimo wa Uganda Vincent Ssempijja

Kwa upande wake, balozi wa Iran nchini Uganda Sayyed Morteza Mortazavi ameashiria uwezo wa mashirikia ya Iran katika nyuga mbalimbali za uchumi hususan sekta ya kilimo na akatoa wito wa kurahisishwa njia za kuyawezesha mashirika hayo kuingia kwenye soko la Uganda.

Mortazavi aidha amemfikishia Waziri wa Kilimo wa Uganda salamu za mwaliko kutoka kwa Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  Mahmoud Hojjati wa kutembelea Iran ili kuja kujionea kwa karibu uwezo wa mashirika ya Kiirani na mafanikio yaliyopata mashirika ya kitaalamu ya Iran katika utumiaji teknolojia za kisasa katika sekta ya kilimo.../