Zarif: Dunia yote inapinga sera hasi za Marekani dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49265
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera hasi na maamuzi yanayokiuka sheria za kimataifa ya Marekani yanakabiliwa na upinzani mkubwa katika kila kona ya dunia, huku Washington ikijiandaa kuanza kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Tehran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 04, 2018 08:01 UTC
  • Zarif: Dunia yote inapinga sera hasi za Marekani dhidi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera hasi na maamuzi yanayokiuka sheria za kimataifa ya Marekani yanakabiliwa na upinzani mkubwa katika kila kona ya dunia, huku Washington ikijiandaa kuanza kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Tehran.

Mohammad Javad Zarif aliyasema hayo jana Jumamosi katika mahojiano na shirika la habari la IRNA pambizoni mwa mkutano wa 18 Baraza la Mawaziri wa Nchi wananchama wa Jumuiya ya Nchi 8 Zinazostawi (D-8) katika mji wa Antalya nchini Uturuki.

Dakta Zarif amesema, aghalabu ya nchi duniani haziungi mkono misimamo ya Marekani haswa tabia yake ya kuziwekea vikwazo vya upande mmoja nchi nyingine. Alkhamisi iliyopita, nchi 189 wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zilipasisha azimio la kuitaka Marekani iiondolee Cuba vikwazo vya zaidi ya miaka 50.

Utawala haramu wa Israel na Ukraine ndizo tu zilizopiga kura ya kutounga mkono azimio hilo. 

Vikwazo vipya vya US vinatekelezwa baada ya Trump kuindoa nchi hiyo JCPOA

Kesho Jumatatu Marekani inatazamiwa kuanza kutekeleza vikwazo vya kibenki na kifedha hasa kuzuia uuzaji wa mafuta ya Iran katika soko la kimataifa.

Tayari mawaziri wa mambo ya nje na fedha wa Ujerumani, Ufaransa na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya wametoa taarifa ya pamoja na kusema wamechukua hatua maalumu za kifedha ili kulinda uhusiano wao wa kibiashara na Iran katika kipindi cha vikwazo vya Marekani.