Larijani: Kundi la kigaidi la Daesh lilianzishwa na Marekani
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa kundi la kigaidi la Daesh lilianzishwa na Marekani na kwamba madai kuwa serikali ya Washington inapambana na ugaidi siyo ya kweli.
Dakta Ali Larijani ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Siasa za Kigeni na Usalama wa Taifa ya Bunge la Brazil, Fernando Collor aliyeko safarini mjini Tehran na kuongeza kuwa, mienendo ya Rais Donald Trump wa Marekani imezusha hali ya mchafukoge katika uga wa kimataifa na kiongozi huyo alidhani kuwa angeweza kuivuruga Iran kwa kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Larijani amesema Trump hajasoma historia na anahitajia ushauri nasaha. Ameongeza kuwa, Iran siyo nchi iliyoundwa baada ya Vita vya Dunia katika karne ya 20 bali ni nchi yenye historia kongwe ya maelfu ya miaka na inaweza kutatua matatizo yake yenyewe.
Spika wa Bunge la Iran ameashiria uhusiano mzuri wa kibiashara uliopo baina ya Tehran na Brasília na kusema: Uhusiano wa Iran na Brazil unaweza kupanuliwa zaidi hususan katika sekta za viwanda na kilimo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Siasa za Kigeni na Usalama wa Taifa ya Bunge la Brazil amesema kuwa Donald Trump haheshimu sheria za kimataifa na kwamba nchi mbalimbali zinapaswa kukabiliana na sera za mabavu na dhulma hususan za Marekani ambayo imevuruga uhusiano wa kimataifa.
Fernando Collor pia amezungumzia mauaji yaliyofanywa na maafisa wa serikali ya Saudi Arabia dhidi ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi na kusema: Marekani imeamua kunyazia kimya mauaji hayo kutokana na biashara ya silaha na Saudia yenye thamani ya dola bilioni 140.