IAEA yathibitisha kwa mara ya 13: Iran inatekeleza kikamilifu JCPOA
(last modified Tue, 13 Nov 2018 03:59:17 GMT )
Nov 13, 2018 03:59 UTC
  • IAEA yathibitisha kwa mara ya 13: Iran inatekeleza kikamilifu JCPOA

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umetoa ripoti yake mpya ya msimu na kuthibitisha kwa mara ya 13 kuwa Iran ingali inatekeleza ahadi na majukumu yake yote katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, amethibitisha kupitia ripoti yake mpya aliyotoa jana kuwa Iran ingali inaendelea kutekeleza majukumu iliyojikubalisha katika makubaliano ya nyuklia.

Amano amesisitiza kuwa Iran haijarutubisha wala kuweka akiba ya urani zaidi ya kiwango ilichoainishiwa na imetoa fursa kamili kwa wakaguzi wa IAEA kukagua vituo vyake vya nyuklia.

Tangu yalipofikiwa makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kati ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1, ambazo ni China, Russia, Uingereza, Ufaransa, Marekani na Ujerumani, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umekuwa ukitoa ripoti mara moja kila baada ya miezi mitatu kuhusu mwenendo wa utekelezaji wa makubaliano hayo na jinsi Iran inavyoendelea kutekeleza makubaliano yenyewe. Katika ripoti zake zote ilizotoa hadi sasa, IAEA imethibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kutekeleza ahadi na majukumu yake kulingana na makubaliano ya JCPOA.

Pamoja na hayo, mnamo tarehe 8 Mei mwaka huu, Donald Trump, rais wa Marekani, ambayo ilikuwa moja ya nchi wanachama wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA alichukua hatua ya upande mmoja na ya ukiukaji makubaliao kwa kutangaza kujitoa nchi yake kwenye makubaliano hayo ya kimataifa sambamba na kuchukua uamuzi wa kuvirejesha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran.

Uamuzi huo wa Marekani wa kujitoa kwenye JCPOA umekosolewa sana duniani hususan na taasisi za kimataifa pamoja na nchi nyingine tano wanachama wa makubaliano hayo ya nyuklia.../

Tags