Rouhani: Marekani haiwezi kukata uhusiano wa Iran na nchi za dunia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani haina uwezo wa kukata uhusiano wa Iran na nchi mbalimbali duniani.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo katika mkusanyiko mkubwa wa wananchi wa Shahrud mkoani Semnan huko mashariki mwa Tehran na kuongeza kuwa, Marekani inapaswa kuelewa kwamba, watu wa Iran watalinda uhusiano wao wa kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa na nchi za kanda hii na dunia na watapanua zaidi mahusiano yao na majirani na nchi za Kiislamu.
Rais Rouhani amesema Marekani na Wazayuni hawawezi kustahamili Iran imara na yenye nguvu, na taifa la Iran kamwe halijawahi kusalimu amri mbele ya adui na wala halitafanya hivyo. Ameongeza kuwa, taifa kubwa la Iran limethibitisha kwamba, ndilo litakalopata ushindi wa mwisho katika vita vyake na Marekani.
Rais wa Iran amesema Marekani inataka kudhoofisha uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine duniani na kuongeza kuwa: Uhusiano wa taifa la Iran na nchi za magharibi yake yaani Iraq na Uturuki, na za kaskazini yaani Jamhuri ya Azerbaijan, Russia, Kazakhstan na Turkumenistan na zile za mashariki ambazo ni Afghanistan na Pakistan na vilevile uhusiano wake na nchi za kusini kama Oman, Qatar na Kuwait ni mzuri na imara zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma, na Marekani haina uwezo wa kuharibu na kukata uhusiano wa Tehran na nchi za kanda hii na dunia.
Amesema kuwa jeshi la Iran, Kiongozi wa Mapinduzi na asasi za utawala wa Kiislamu hapa nchini zinawasaidia watu wa kanda hii ya Mashariki ya Kati kwa ajili ya kudhamini usalama wa nchi za Iraq,Syria na Lebanon na kwamba Jamhuri ya Kiislamu pia inafanya bidii kuwasaidia katika vita vya kijeshi na kisiasa watu wanaodhulumiwa wa Yemen mbele ya wavamizi wa utawala wa Aal Saud.