Maafisa wa Iran na Misri wajadili masuala ya pande mbili
Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa, Hossein Amir-Abdollahian amekutana hapa mjini Tehran na kufanya mazungumzo na afisa mkuu anayeshughulikia maslahi ya Misri hapa nchini, Yasser Othman ambapo wamesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa na mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Misri wamezungumzia masuala yenye maslahi ya pande mbili, likiwemo suala la kuimarisha ushirikiano wa kibunge wa Cairo na Tehran.
Maafisa hao wa Iran na Misri wamesisitiza kuwa, ushirikiano wa mabunge ya nchi mbili hizi unaweza kuwa kigezo katika kuipatia ufumbuzi migogoro inayolikabili eneo hili, hususan ufumbuzi wa kisiasa.
Aidha wawili hao wamesisitizia haja ya kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali, sanjari na kuweko ushirikiano wa dhati na wa kivitendo wa kupambana na jinamizi la ugaidi.
Kadhalika maafisa hao wa ngazi za juu wa Iran na Misri wamejadili masuala muhimu ya kieneo, haswa kadhia ya Palestina, ambapo wamesisitizia udharura wa kuendelea kulitetea na kuliunga mkono taifa huru la Palestina.