Zarif: Iran itaendelea daima kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50507-zarif_iran_itaendelea_daima_kuunga_mkono_malengo_matukufu_ya_palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Jamhuri ya Kiislamu itaendelea daima kuwa bega kwa bega na watu wa Palestina na kuyaunga mkono malengo yao matukufu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2018 23:22 UTC
  • Zarif: Iran itaendelea daima kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Jamhuri ya Kiislamu itaendelea daima kuwa bega kwa bega na watu wa Palestina na kuyaunga mkono malengo yao matukufu.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo mjini Tehran katika mazungumzo na Ziad al-Nakhala, Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina. Zarif ameongeza kuwa: Kuiunga mkono na kuihami Palestina ni moja ya misingi mikuu ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina ametoa shukrani kwa watu wa Iran kutokana na uungaji mkono wao kwa Palestina na akaeleza kwamba: Iran ni miongoni mwa waungaji mkono wa kweli wa malengo matukufu ya Palestina.

Waziri Zarif (kushoto) akimlaki Katibu Mkuu wa Jihadul-Islami ya Palestina na ujumbe aliofuatana nao

Al-Nakhala ameashiria hatua za baadhi ya nchi za Kiarabu na za Magharibi za kutaka kutoa pigo la kuudhuru muqawama, na akasisitiza kwamba: Wananchi wa Palestina wana azma thabiti zaidi hivi sasa kuliko walivyokuwa huko nyuma ya kuendeleza njia ya muqawama hadi ushindi kamili.

Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amebainisha pia kwamba, muqawama umekomaa na una uwezo wa juu zaidi hivi sasa kuliko ulivyokuwa huko nyuma kwa ajili ya kukabiliana na uchokozi; na akaongeza kwamba: Matunda ya uwezo na ukomavu huo yameonekana katika maandamano ya Haki ya Kurejea na kusambaratishwa kwa uvamizi wa karibuni uliofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Maandamano ya amani ya "Haki ya Kurejea" yalianza tarehe 30 Machi katika mpaka wa Ukanda wa Gaza kwa mnasaba wa "Siku ya Ardhi" na hadi sasa yangali yanaendelea.../