Iran yajibu tuhuma za Saudia na Utawala wa Kizayuni
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa jibu kali kwa matamshi yasiyo na msingi ya mabalozi wa Utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudia dhidi ya Iran.
Siku ya Alkhamisi, Saudia ilishirikiana na utawala wa Israel kutoa tuhuma za kukaririwa dhidi ya Iran na kudai kuwa eti Jamhuri ya Kiislamu ni tishio kwa usalama wa kimataifa.
Katika kujibu tuhuma hizo zilizotolewa katika kikao cha Baraza la Usalama, Jawad Safai mwanadiplomasia mwandamizi wa Iran katika Umoja wa Mataifa alisema: "Utawala wa Kizayuni wenyewe ni muungaji mkono wa ugaidi duniani. Utambulisho wa utawala huo ni wa kigaidi tokea kuanzishwa kwake na umehusika na mauaji ya maelfu ya wapinzani wake wakiwemo Wairani 17 elfu hasa wataalamu wa nyuklia. Aidha utawala ghasibu Israeli umehusika na ukatili mbaya zaidi dhidi ya Wapalestina kwa kuwadondoshea mabaomu kwa zaidi ya miongo sita sasa. Mwakilishi wa utawala huo anapaswa kuwa mtu wa mwisho kuzungumza kuhusu vita dhidi ya ugaidi."
Mwanadiplomasia huyo wa Iran pia amejibu madai ya mwakilishi wa Saudia kwa kusema: "Kutoa tuhuma dhidi ya Iran ni njama ya kupotosha fikra za walimwengu kuhusu utambulisho wa Saudi Arabia kama chimbuko la ugaidi, misimamo mikali na idiolojia ya ukufurushaji ambayo ni kiini cha oparesheni zote za hivi karibuni za kigaidi. Saudia ni chanzo hatari zaidi cha machafuko Mashariki ya Kati na kote duniani na inachochoea pia vita vya kimadhehebu."
Mwakilishi huyo wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashiriki kikamilifu katika harakati zote za vita dhidi ya ugaidi.