Spika Larijani: Magaidi ni jeshi la Marekani Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51229-spika_larijani_magaidi_ni_jeshi_la_marekani_mashariki_ya_kati
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge la Iran) amesema kuwa Marekani sasa inawahamisha magaidi kuwatoa sehemu moja na kuwapeleka sehemu nyingine baada ya kuwatumia kama wenzo wa kutimiza malengo yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 31, 2019 01:02 UTC
  • Spika Larijani: Magaidi ni jeshi la Marekani Mashariki ya Kati

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge la Iran) amesema kuwa Marekani sasa inawahamisha magaidi kuwatoa sehemu moja na kuwapeleka sehemu nyingine baada ya kuwatumia kama wenzo wa kutimiza malengo yake.

Spika Ali Larijani aliyasema hayo jana katika mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Nje ya Bunge la Algeria aliyeko safarini mjini Tehran. Amesema kuwa, Marekani hairuhusu kutokomezwa magenge ya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, magaidi hao wanavuruga eneo hilo kwa mujibu wa siasa na sera za serikali ya Washington na sasa yameelekeza harakati zao katika baadhi ya maeneo ya Asia na kaskazini mwa Afrika.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia mpango wa Kimarekani wa "Muamala wa Karne" kuhusu kadhia ya Palestina na kusema kuwa, Wamarekani wanataka kulibana suala la Palestina na kulihusisha tu na Ukanda wa Gaza, na huu ni usaliti mkubwa. 

Dakta Larijani amesema mpango wa kutaka kujenga uhusiano baina ya utawala ghasibu wa Israel na nchi za Kiarabu ni doa jeusi kwa nchi za Kiislamu na kuongeza kuwa, mpango huo hautafanikiwa kutokana na mwamko uliopo sasa baina ya mataifa ya Waislamu.

Ujumbe wa Bunge la Algeria mjini Tehran

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Nje ya Bunge la Algeria, Abdelhamid Si Afif amekosoa ulingiliaji wa madola ya kibeberu katika masuala ya ndani ya nchi za Kiislamu na kusema kuwa: Hakuna mtu anayeweza kuifundisha Algeria ifanye nini katika uhusiano wake na nchi ndugu na rafiki. 

Abdelhamid Si Afif ametilia mkazo udharura wa kupanuliwa zaidi uhusiano wa kiuchumi wa Tehran na Algiers na kusema Algeria inalaani vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran na inataka kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.