Iran: Hatukwamishwi na chochote katika kuimarisha nguvu zetu za makombora + Video
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51311-iran_hatukwamishwi_na_chochote_katika_kuimarisha_nguvu_zetu_za_makombora_video
Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kwa kusisitiza kwamba, leo hii Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina matatizo yoyote ya kiufundi wala ya kiteknolojia katika kustawisha nguvu zake za makombora.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 03, 2019 12:48 UTC
  • Iran: Hatukwamishwi na chochote katika kuimarisha nguvu zetu za makombora + Video

Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kwa kusisitiza kwamba, leo hii Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina matatizo yoyote ya kiufundi wala ya kiteknolojia katika kustawisha nguvu zake za makombora.

Brigedia Jenerali Hussein Salami amesema hayo katika mohojiano maalumu aliyofanywa na Kanali ya Pili ya televisheni ya Iran na kuongeza kuwa, kustawisha na kuimarisha nguvu za makombora ni kitu muhimu sana kwa Iran katika stratijia yake ya kuzuia kushambuliwa.

 

Amesema, nguvu hizo zinaimarishwa kwa kuzingatia tu matakwa ya taifa kubwa la Iran na ni katika siasa kuu za Iran ambazo zimebainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Brigedia Jenerali Salami amegusia pia chokochoko na uvumi ulioenezwa hivi karibuni na nchi za Ulaya kuhusu mradi wa ulinzi wa makombora wa Iran na kusema kuwa, nguvu na uwezo wa makombora ya Iran ni haki ya kiulinzi na kiusalama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo manifesto na mkakati wake mkuu ni kuzuia kushambuliwa.

 

Kaimu Kamanda huyo wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH vile vile amesema, kama nchi za Ulaya au mtu mwingine yeyote atajaribu kuendesha njama za kujaribu kuipokonya Jamhuri ya Kiislamu silaha zake hizo muhimu, jambo hilo litaifanya Iran ifikirie kufanya mabadiliko muhimu sana kiistratijia.

 

Vile vile amesema, lau kama Iran isingeliitikia maombi ya nchi mbili za Iraq na Syria zilizoiomba izisaidie katika kupambana na magaidi, basi leo hii nchi za Ulaya zingelikuwa katika machafuko na ukosefu wa amani.