Rouhani: Magaidi hawapaswi kuachiwa wajihisi wako salama katika kona yoyote ya dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51566-rouhani_magaidi_hawapaswi_kuachiwa_wajihisi_wako_salama_katika_kona_yoyote_ya_dunia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, lengo la pamoja la nchi za Iran, Russia na Uturuki katika kupambana vilivyo na ugaidi ni kurejesha usalama na utulivu nchini Syria na kuongeza kuwa, magaidi hawapaswi kuhisi wako salama katika kona yoyote ile ya dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 15, 2019 04:34 UTC
  • Rouhani: Magaidi hawapaswi kuachiwa wajihisi wako salama katika kona yoyote ya dunia

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, lengo la pamoja la nchi za Iran, Russia na Uturuki katika kupambana vilivyo na ugaidi ni kurejesha usalama na utulivu nchini Syria na kuongeza kuwa, magaidi hawapaswi kuhisi wako salama katika kona yoyote ile ya dunia.

Rais Rouhani amesema hayo katika kikao cha pande tatu za Iran, Russia na Uturuki kilichomalizika jana mjini Sochi, Russia na kuwaambia waandishi wa habari mwisho mwa kikao hicho kwamba: miongoni mwa masuala yaliyotiliwa mkazo katika kikao hicho ni wajibu wa kupambana na ugaidi katika maeneo yaliyobakia ya Syria ikiwemo Idlib. Amesema nchi zote hizo tatu zina mtazamo mmoja kwamba idlib ni sehemu ya ardhi ya Syria na kuna wajibu wa kusafishwa maeneo hayo na uchafu wa magaidi bila ya kujali majina yao.

Marais wa Iran, Russia na Uturuki (kutoka kushoto kwenye kulia)

 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, njia pekee ya kutatua mgogoro wa Syri'a ni mazungumzo ya kisiasa na kamwe si njia ya kijeshi na kufafanua kuwa, Iran, Russia na Uturuki zina hamu ya kuona usalama na amani kamili inarejea nchini Syria sambamba na kustawishwa zaidi na zaidi ushirikiano na serikali ya Rais Bashar al Assad inayotawala kihalali na kwa mujibu wa katiba ya nchi hiiyo.

Kikao cha siku moja cha Sochi huko Russia kilifanyika jana Alkhamisi kikiwakutanisha pamoja marais wa Iran, Russia na Uturuki ajenda yake kuu ikiwa ni kupambana na ugaidi wa kieneo, kurejesha utulivu, kuwarejesha nyumbani wakimbizi na kuleta utulivu wa kisiasa nchini Syria.

Rais Rouhani mapema leo asubuhi amerejea hapa nchini akitokea kwenye kikao hicho cha siku moja.