Feb 20, 2019 02:42 UTC
  • SEPAH: Magaidi watatu wa shambulizi la Zahedan ni raia wa Pakistan

Kamanda wa kikosi cha nchi kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran amesema kuwa, gaidi aliyejilipua kwa bomu na wenzake wawili kati ya waliohusika na shambulizi la kigaidi lililofanyika siku chache zilizopita dhidi ya askari wa jeshi hilo katika mkoa wa Sistan na Baluchestan wametambuliwa kuwa ni raia wa Pakistan.

Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour amesema gaidi aliyejilipua kwa gari lililolenga basi la askari wa kikosi cha SEPAH anajulikana kwa jina la Hafiz Mohammad Ali na yeye na wenzake wawili waliotiwa nguvuni ni rais wa Pakistan.

Ameongeza kuwa baada ya uchunguzi wa gari lililotumiwa katika shambulizi hilo la kigaidi kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kilianza opesheni ya kuwatia nguvuni magaidi hao na kusambaratisha timu yao. Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour amesema kuwa, katika operesheni hiyo askari usalama wa Iran wamefanikiwa kumtia nguvuni gaidi mmoja mwanamke na magaidi wengine wawili na kwamba, mwanachama mwingine mmoja wa genge hilo ametoroka na anafuatiliwa na vyombo vya usalama. 

Amesema kuwa genge hilo la kigaidi lilikuwa na zana nyingi za kivita na kwamba lilikuwa na nia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi hapa nchini katika maadhimisho ya miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu tarehe 11 Februari lakini walishindwa kufanya hivyo.    

Mahmoud Alavi

Wakati huo huo Waziri wa Usalama wa Iran, Mahmoud Alavi amesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali kwa wahalifu waliohusika na shambulizi hilo la kigaidi.

Ikumbukwe kuwa, Jumatano iliyopita ya Februari 13, basi lililokuwa limewabeba askari walinda mpaka wa Iran lilishambuliwa na magaidi lilipokuwa likipita katika barabara ya Khash-Zahedan katika mkoa wa Sistan na Baluchistan, kusini mashariki mwa Iran, ambapo askari 27 waliuawa shahidi na wengine 13 kujeruhiwa.

Kundi la kigaidi linalojiita "Jayshul Adl" lilidai kuhusika na hujuma hiyo. Kundi hilo lina mfungamano mkubwa na magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na kufadhiliwa na Saudi Arabia.

Tags