Zarif: Nchi za Magharibi si wachukua maamuzi wakuu
(last modified Sun, 24 Feb 2019 14:16:27 GMT )
Feb 24, 2019 14:16 UTC
  • Zarif: Nchi za Magharibi si wachukua maamuzi wakuu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema nchi za Magharibi zimehatarisha usalama wa Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) kupitia mauzo ya silaha kwa nchi za Kiarabu. Amesema kuwa silaha hizo za nchi za Magharibi zimechangia kuvuruga usalama wa kieneo.

Akizungumza katika kikao cha sera za kigeni katika Chuo Kikuu cha Tehran leo asubuhi, Zarif amesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, nchi za Magharibi zimeziuzia nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi silaha zenye thamani ya dola bilioni 100. Baraza hilo linajumuisha Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kwingineko katika hotuba yake, Zarif amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 nchini Iran yalihitimisha uingiliaji wa madola ya kigeni katika mambo ya ndani ya Iran.

Ndege ya kivita ya utawala wa Saudia aina ya Tornado iliyonunuliwa kutoka Uingereza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha zaidi kuwa, nchi za Magharibi si wahusika wakuu tena katika maamuzi muhimu duniani. Amesema hivi sasa dunia iko katika zama za baada ya satwa ya madola ya Magharibi huku akiongeza kuwa,  nchi zote duniani zinapaswa kuchukua muelekeo wa uchukuaji maamuzi ya pamoja katika hali ya hivi sasa. Zarif amesisitiza pia ulazima wa kutumiwa udipliomasia sambamba na uwezo wa kijeshi na kuongeza kuwa Iran pia inafuata msingi huo na imeweza kufikia malengo yake.

 

Tags