Wabunge wa Iran wakusanya sahihi kumsihi Zarif asijiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51828-wabunge_wa_iran_wakusanya_sahihi_kumsihi_zarif_asijiuzulu
Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) wameanza kukusanya sahihi kwa shabaha ya kumuomba Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aghairi msimamo wake wa kujiuzulu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 27, 2019 08:00 UTC
  • Wabunge wa Iran wakusanya sahihi kumsihi Zarif asijiuzulu

Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) wameanza kukusanya sahihi kwa shabaha ya kumuomba Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aghairi msimamo wake wa kujiuzulu.

Ali Najafi Khoshroudi, Msemaji wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje ya Bunge la Iran amesema zaidi ya wabunge 150 wa Majlisi ya Ushauri wametia saini waraka huo wa kumuomba Mohammad Javad Zarif asijiuzulu.

Kikao cha wazi cha Bunge la Iran kilifanyika jana Jumanne chini ya uenyekiti wa Spika Ali Larijani, ambapo wabunge 199 walihudhuria. 

Haya yanajiri katika hali ambayo, Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Rais Hassan Rouhani hajalikubali ombi la Dakta Zarif kujiuzulu.

Usiku wa kuamkia jana Jumanne, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif alitangaza kujiuzulu ghafla kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Rais Rouhani na Bijan Namdar Zanganeh, Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Wakati huohuo, Tehran imepuuzilia mbali na kuitaja kama uvumi na tetesi, habari ya kujiuzulu Bijan Namdar Zanganeh, Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kasra Nouri, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhusiano Mwema cha wizara hiyo amesema kuwa, "Waziri Zanganeh hajiuzulu, atachukua uamuzi kwa mambo yenye maslahi kwa nchi na taifa lake."