Rais Rouhani azuru nyumba ya Imam Khomeini MA mjini Najaf Iraq + Video
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo jioni ametembelea eneo la kihistoria na kiutamaduni ambalo ni nyumba ya kihistoria ya Imam Khomeini MA mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu mjini Najaf Iraq na kukumbuka siku ambazo Imam Khomeini aliishi kwa mashaka katika nyumba hiyo baada ya mfalme wa Iran kumbaidishia Iraq mwanachuoni huyo mwanamapambano.
Kabla ya hapo pia, Rais Rouhani alikuwa amemtembelea Ayatullah Ali Sistani, marjaa wa Waislamu wa Kishia mjini Najaf huko Iraq.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbali na kumjulisha Ayatullah Sistani mafanikio yaliyopatikana katika safari yake ya kuitembelea Iraq na kuonana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo, ametilia mkazo pia kuimarisha uhusiano wa kiudugu na ujirani mwema baina ya mataifa haya mawili ndugu.
Kwa upande wake Ayatullah Sistani amesisitiza kuwa anaunga mkono juhudi zozote zile za kustawisha uhusiano wa Iraq na majirani zake kwa kuzingatia maslahi ya pande mbili na kuheshimiana.
Ayatullah Sistani vile vile amehimiza mapambano dhidi ya ufisadi, kuimarishwa huduma za jamii na kuhakikisha kuwa, silaha zinabakia mikononi mwa serikali na taasisi za usalama tu akielezea matumaini yake kwamba serikali ya Iraq itaweza kulifanikisha jukumu lake hilo.
Kabla ya hapo Rais Rouhani alisema wakati alipoonana na Rais Barham Salih wa Iraq hiyo jana kwamba, usalama na utulivu wa Iraq una umuhimu mkubwa kwa Iran kwani Iraq yenye utulivu inaweza kuwa na nafasi muhimu katika eneo hili.
Vile vile alisema wakati alipohutubia kikao cha wasomi wa Iraq hiyo jana kwamba "Watu wote wanajua kuwa, madola ya Magharibi hayajahusika hata kidogo katika jitihada za kuangamizwa magaidi katika eneo la Asia Magharibi na walirusha ndege na helikopta zao angani kimaonyesho tu.