Iran yalalamikia hatua ya Kenya, yamwita nyumbani balozi wake Nairobi kwa mashauriano
Balozi wa Kenya mjini Tehran ameitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kukabidhiwa malalamiko ya Jamhuri ya Kiislamu kuhusu ukiukaji wa haki za wafungwa wawili Wairani wanaoshikilia nchini Kenya.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi amesema kuwa, balozi wa Kenya mjini Tehran Bi Rukia Subow ameitwa na kukabidhiwa malalamiko ya Iran kufuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kilele ya Kenya wa kubatilisha hukumu ya kuachiwa huru raia hao wawili wa Iran iliyokuwa imetolewa na Mahaka ya Rufaa.
Bahram Qassemi ameongeza kuwa, katika mazungumzo yake na balozi Subow, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika ameeleza kutofurahishwa Jamhuri ya Kiislamu na uamuzi usiyo wa kiadilifu uliotolewa na mahakama ya Kenya na amemjulisha kwamba, Iran imemwita nyumbani balozi wake nchini Kenya kwa ajili ya mashauriano.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Balozi Rukia Subow pia ameahidi kuwasilisha malalamiko hayo kwa serikali ya Nairobi.
Bahram Qassemi amesema kuwa, Februari mwaka 2018 Mahakama ya Rufaa ya Kenya ilisikiliza tena kesi inayowahusu raia hao wawili wa Iran na kutoa uamuzi kwamba hawakuwa na hatia yoyote na waachiwe huru. Hata hivyo baada ya uingiliaji kati usio wa kisheria, polisi ya Kenya ilizuia kuachiwa huru Wairani hao.
Qassemi amesema Mahakama ya Kilele ya Kenya Ijumaa iliyopita ilibatilisha uamuzi wa Mahaka ya Rufaa na kusema Wairani hao wawili wanapaswa kurejeshwa jela.