Mar 21, 2019 03:54 UTC
  • Kiongozi Muadhamu autangaza Mwaka 1398 Shamsiya kuwa mwaka wa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe kwa munasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1398 Hijiria Shamsia, ametuma salamu za pongezi za Nowuruz (Nairuzi) na pia salamu kwa munasaba wa Wilada ya Imam Ali AS kwa wananchi wa Iran na hasa familia za mashahidi na majeruhi wa vita na amelitakia taifa la Iran mwaka wenye furaha, saada, afya ya kimwili na mafanikio ya kimaada na kimaanawi na ameutaja mwaka mpya kuwa mwaka wa "kustawi uzalishaji".

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika tathmini yake kuhusu mwaka 1397 Hijria Shamsia uliopita, ameutaja kuwa mwaka  uliojaa pandashuka nyingi na kusema:  "Katika mwaka huo, adui alipanga njama nyingi dhidi ya Iran lakini taifa la Iran, liliweza kunawiri kwa maana halisi ya neno hilo na hivyo, kwa nguvu, muono wa mbali na hima ya vijana, njama hizo zimesambaratishwa."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema taifa la Iran limetoa jibu imara na lenye nguvu kwa vikwazo shadidi vya Marekani na Ulaya katika nyuga za kisiasa na kiuchumi. Ameongeza kuwa: "Katika uga wa kisiasa, dhihirisho la wazi la jibu hilo ni maandamano makubwa ya 22 Bahman (11 Februari) na misimamo ya wananchi katika kipindi chote cha mwaka. Katika uuga wa makabiliano ya kiuchumi pia,  taifa la Iran limeweza "kuongeza ubunifu wa kisayansi na kiufundi", "kuimarisha kwa kiwango kikubwa mashirika ambayo msingi wake ni elimu", kuimarisha uundwaji wa miundo msingi ya ndani ya nchi kama vile kufunguliwa awamu kadhaa za vituo vikubwa vya uzalishaji gesi asilia kusini mwa nchi na kufunguliwa kituo kikubwa cha usafishaji mafuta cha Bandar Abbas."

Kiongozi Muadhamu amesema kwa hatua hizo za uga wa uchumi, taifa la Iran limeweza kukabiliana na uhasama na ukhabithi wa maadui  na hivyo kuonyesha nguvu na adhama yake  na kwa msingi huo kuimarisha hadhi na heshima ya taifa, Mapinduzi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei ameendelea kusema kuwa,  tatizo kuu la nchi linaendelea kuwa tatizo la kiuchumi na huku akiashiria kuongezeka matatizo ya kimaisha ya wananchi katika miezi ya hivi karibuni amesema: "Sehemu ya matatizo hayo inatokana na usimamizi usio sahihi katika uga wa masuala ya kiuchumi na hilo linapaswa kufidiwa." Amesema ingawa kuna mipango na tadbiri ya kukabiliana na matatizo hayo, tadbiri hiyo inapaswa kuzaa matunda katika mwaka mpya na wananchi wahisi taathira yake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna wananchi wa Iran waliovyoukaribisha mwaka uliopita wa 97 kwa kauli mbiu ya "Kuunga Mkono Bidhaa za Iran" , na athari chanya za kauli mbiu hiyo na kusema: "Mwaka huu, suala  la kimsingi ni " Uzalishaji" kwani iwapo uzalishaji utakuwepo, matatizo ya kimasiha na ajira yataweza kutatuliwa na pia nchi haitakuwa tegemezi kwa  maajinabi  na maadui na hata jambo hilo linaweza kwa kiwango kikubwa kutatua tatizo la thamani ya sarafu ya kitaifa. Kwa msingi huo naitangaza nara na kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni "Kustawi Uzalishaji".

Ayatullah Khamenei ametoa wito kwa wote kujitahidi katika kustawisha uzalishaji nchini na ameelezea matumaini yake kuwa, kwa kuimarika na kuboreka uzalishaji mwaka huu, matatizo ya kiuchumi yatachukua mkondo wa utatuzi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametuma salamu kwa roho toharifu ya Imam Khomieni MA na mashahidi watukufu, na salamu kwa Imam Waliul Asr- Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake- na amemuomba Mwenyezi Mungu SWT alijaalie saada taifa la Iran na mataifa yote yanayoadhimisha Nowruz. 

Tags