Apr 16, 2019 06:58 UTC
  • Iran: Kwa mara nyingine Marekani imedhihirisha udhalili wake

Msemaji wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, hatua ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya ya kuzuia kutumwa misaada ya nchi nyingine kwa ajili ya wahanga wa mafuriko nchini Iran, imedhihirisha udhalili wake wa kukabiliana na ubinaadamu na haki za msingi za kibinaadamu.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami aliyasema hayo jana mbele ya waandishi wa habari baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wnaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kwamba hata nchi ambazo zinashuhudia vita huwa zinashirikiana na nchi nyingine katika suala zima la utumaji misaada ya kibinaadamu, lakini Marekani na washirika wake kwa mara nyingine zimeonyesha udhalili wao katika suala la ufikishaji misaada kwa wahanga wa mafuko nchini Iran.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami, Msemaji wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ameashiria wendawazimu wa Marekani katika kulitaja Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH (IRGC) kuwa la kigaidi na kusema kuwa hatua hiyo pia ni ya kidhalili na kwamba, majeshi ya Iran pamoja na jeshi la IRGC yamekuwa yenye kupendwa nchini hapa. Amesisitiza kwamba harakati hiyo ya Marekani imezidisha zaidi mapenzi ya wananchi kwa majeshi hayo. Mvua nyingi ambazo zimekuwa zikinyesha katika maeneo ya kaskazini, magharibi na kusini mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimesababisha hasara nyingi za kifedha na kiroho na kwa mujibu wa idara ya afya nchini Iran jumla ya watu 76 wamepoteza maisha yao katika matukio hayo. 

Tags