Rouhani: Njama za Marekani dhidi ya Iran zitashindwa + Video
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Wamarekani katika kipindi cha miaka 40 sasa wamekuwa wakipanga njama kila siku dhidi ya taifa la Iran na katika muda huo wote wamekuwa wakishindwa."
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri na kusisitiza kuwa: "Hadi sasa, Marekani imeshindwa katika sera na propaganda zake dhidi ya Iran kieneo na kimataifa." Ameendelea kusema kuwa: "Taifa la Iran litasimama kidete katika kukabiliana na hatua zilizo kinyume cha sheria za Marekani."
Rais Rouhani amebaini kuwa, Marekani itajuta kutokana na hatua zake za kidhalimu na zilizo kinyume cha sheria. Aidha amesema: "Wavamizi ambao wanataka kuliwekea mashinikizo taifa la Iran wanapaswa kufahamu wamechagua mkondo ghalati na usio sahihi."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kutaka kuhakikisha kuwa uuzaji wa mafuta ghafi ya petroli ya Iran katika soko la kimataifa unafika sufuri ni jambo lisilowezekana. Ameongeza kuwa: "Iran ina njia mbali mbali za kuuza mafuta yake."
Rais Rouhani aidha ameashiria namna baadhi ya nchi za eneo zinavyoshirikiana na Marekani katika kuzuia uuzaji wa mafuta ya Iran katika soko la kimataifa na kusema: "Saudi Arabia na Imarati zifahamu kuwa, kuendelea kuwepo kwao kunatokana na maamuzi ya busara yaliyochukuliwa na Iran kwani kama si hatua ambazo Jamhuri ya Kiislamu ilizichukua, Saddam, diktetea aliyepinduliwa wa utawala wa Baath Iraq angekuwa ameshateka na kukalia kwa mabavu Riyadh na Abu Dhabi."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria uhusiano mzuri wa Iran na aghalabu ya nchi jirani na kusema: "Baadhi ya nchi jirani ambazo zinashirikiana na Marekani katika kufikia malengo yake yaliyo dhidi ya Iran zifahamu kuwa, zama za utawala wa Trump zitafika ukingoni na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kubakia na kudumu."