Zarif: Vikwazo havitabadilisha sera za Iran
(last modified Thu, 25 Apr 2019 03:42:47 GMT )
Apr 25, 2019 03:42 UTC
  • Zarif: Vikwazo havitabadilisha sera za Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hazitabadilishwa kwa vikwazo."

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo Jumatano katika kikao cha "Jumuiya ya Asia mjini New York' ambapo amekosoa sera za undumakuwili za Marekani duniani na kusema: "Rais Donald Trump wa Marekani amejiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na mikataba mingine ya kimataifa jambo ambalo limepelekea nchi zingine zisiweze kuwaamini tena Wamarekani."

Zarif amesema hadi sasa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umeshatoa ripoti 14 mtawalia ambazo zinaonyesha Iran inafungamana na ahadi zake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kuwa: "Wakuu wa Marekani hawawezi kuzlilazimisha nchi zifuate matakwa yao."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha ameashiria namna ambavyo nchi za Ulaya hazijatekeleza ahadi zao katika mapatano ya JCPOA baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa na kusema: " Mfumo biashara wa INSTEX ni sehemu ya ahadi za nchi za Ulaya na Iran bado inasubiri utekelezwe." 

Nchi za Ulaya zinalenga kutumia mfumo huo wa kifedha unaojulikana kama INSTEX ili kulinda manufaa ya kiuchumi ya mapatano ya JCPOA kwa maslahi ya Iran.

Zarif ameashiria kuhusu kufungwa Lango Bahari la Hormoz na kusema: "Ghuba ya Uajemi ni mshipa wa uhai wa dunia na maadamu maslahi ya kitaifa ya Iran yanalindwa Hormoz itabakia kuwa wazi."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria pia jitihada za Marekani za kuizuia Iran iuze mafuta yake katika soko la dunia na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuuza mafuta kwani ina wateja wake." Aidha amesema historia imeonyesha kuwa taifa la Iran kamwe halisalimu amri kwani heshima ya Wairani haiwezi kuuzwa.

Tags