Rouhani: Iran itaendelea kuuza mafuta licha ya mashinikizo ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53193-rouhani_iran_itaendelea_kuuza_mafuta_licha_ya_mashinikizo_ya_marekani
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitasimamisha uuzaji wa mafuta yake nje ya nchi licha ya mashinikizo na vikwazo vipya vya Marekani, na kusisitiza kuwa Tehran ina njia za kuuza mafuta yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 30, 2019 07:57 UTC
  • Rouhani: Iran itaendelea kuuza mafuta licha ya mashinikizo ya Marekani

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitasimamisha uuzaji wa mafuta yake nje ya nchi licha ya mashinikizo na vikwazo vipya vya Marekani, na kusisitiza kuwa Tehran ina njia za kuuza mafuta yake.

Rais Rouhani amesema hayo hii leo hapa Tehran, katika marasimu ya kuadhimisha Wiki ya Wafanyakazi na kubainisha kuwa, azma ya Washington ya kutaka kukata kimilifu uuzaji wa mafuta ya nchi hii kamwe haitatimia na kwamba katika miezi ijayo, Marekani haitakuwa na jingine ghairi ya kutazama tu namna nchi hii itakavyoendelea kuyauza mafuta yake nje ya nchi.

Amesema, "Washington imechukua uamuzi ghalati wa kujaribu kufanya uuzaji wamafuta ya Iran ufikie kiwango cha sifuri, hatutaruhusu hilo lifanyike. Tuna njia zetu nyingi za kuendelea kuuza mafuta nje ya nchi ambazo Marekani haizitambui."

Dakta Rouhani ameongeza kuwa, "Lengo kuu la Marekani la kuiwekea Iran vikwazo vya kikatili ni kutaka kufuta mapato ya nje ya taifa hili, lakini kwa uwezo wa Allah, tutaipigisha magoti Marekani."

Amesisitiza kuwa, kusimama kidete dhidi ya Washington ndio wajibu na jukumu kuu la serikali na taifa la Iran.

Uzalishaji mafuta nchini Iran

Aprili 22, Ikulu ya Marekani (White House) iliziagiza nchi nane ambazo zilikuwa zimeruhusiwa na Washington kuendelea kununua mafuta ya Iran licha ya vikwazo vya US ziache kuagiza bidhaa hiyo kuanzia Mei Mosi, vinginevyo zitawekewa vikwazo.

Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa, hakuna mtu anayeweza kuzuia uuzaji wa mafuta yake nje ya nchi; huku China, Uturuki na baadhi ya wateja wengine wakubwa wa mafuta ya Iran wakipinga vikwazo hivyo vya Marekani vitavyoanza kutekelezwa kesho Jumatano.