Larijani: Hatua zinazochukuliwa na Marekani dhidi ya Iran zinaonesha kuchanganyikiwa Washington
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa hatua zinazochukuliwa na Marekani dhidi ya Iran zinaonesha kuchanganyikiwa viongozi wa nchi hiyo na hawajui cha kufanya.
Dk Ali Larijani amesema hayo katika kikao cha leo cha wazi cha Bunge na kuongeza kuwa, hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na utawala wa kibeberu wa Marekani dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kuongeza baadhi ya vikwazo vyake kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran licha ya kwamba ni ya amani kikamilifu, ni njama za Washington za kuzusha vurugu duniani.
Amesema, viongozi wa Marekani wanaendesha vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran lakini vita hivyo vitashindwa tu kama ilivyojiri huko nyuma.
Tarehe 22 mwezi uliopita wa Aprili 2019, serikali ya Marekani ilitangaza kuwa, haitoongeza muda wa msamaha wa kununua mafuta ya Iran kwa wanunuzi wakuu wa bidhaa hiyo muhimu.
Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani alisema, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zimemuahidi kujaza nafasi ya mafuta ya Iran katika soko la dunia.
Ni jambo lililo wazi kuwa ndoto hiyo ya maadui wa taifa la Kiislamu la Iran ni muhali kutimia na wataalamu mbalimbali wanasema hakuna anayeweza kuchukua nafasi ya mafuta ya Iran katika soko la dunia.
Hivi karibuni pia, Katibu Mkuu wa OPEC, Mohammed Sanusi Barkindo, alisema pambizoni mwa Maonyesho ya 24 ya Mafuta, Gesi na Petrokemikali ya Iran hapa Tehran kwamba: "Changamoto kuhusu mafuta ya Iran si ya nchi moja tu bali hata OPEC nayo inaathirika." Aliongeza kuwa, "Kile kinachofanyika Iran, Venezuela na Libya kitakuwa na taathira hasi katika soko na sekta ya mafuta. Tumekuwa na changamoto nyingi katika kipindi cha miaka 60 iliyopita ndani ya OPEC, lakini changamoto zote hizo tumekuwa tukazipatia ufumbuzi kwa ushirikiano."