Zarif: Iran haitafanya mazungumzo na Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema maadamu Marekani haitekelezi ahadi zake katika mapatano ya JCPOA, na maadamu haiiheshimu Iran, basi hakuna mazungumzo yatakayofanyika.
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo katika mahojiano na Televisheni ya CNN ya Marekani na kusisitiza bayana kuwa: "Jamhuri yaKiislamu ya Iran haitafanya mazungumzo na serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani."
Zarif aidha ametahadharisha kuhusu hatua za kichochezi ambazo Marekani imechukua katika eneo la Asia Magharibi na kusema: "Kwa kuongeza askari wake katika eneo, Marekani imeanzisha mchezo hatari sana."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amekosoa hatua ya Marekani kutuma katika eneo la Asia Magharibi ndege za kivita za B-52 zenye uwezo wa kubeba mabomu ya nuklia na meli zake za kivita zinazoongozwa na manowari ijulikanayo kama USS Abraham Lincoln yenye uwezo wa kubeba ndege za kivita. Zarif amesema kutuma zana hizo zote za kivita katika eneo ndogo ni jambo linaloweza kuandaa mazingira ya matukio yenye kuleta maafa.
Kwingineko katika ujumbe wake wa hivi karibuni wa Twitter ikiwa ni katika kujibu vitisho vya Rais Trump, Zarif alimwambia rais huyo mwanagenzi wa Marekani kuwa, asijaribu kumtolea vitisho Muirani yeyote yule.

Zarif amesema "Wairani wamesimama kidete kulinda heshima zao kwa maelfu ya miaka na wavamizi wote wameshindwa na kukimbia. Ugaidi wa kiuchumi na majigambo ya kufanya mauaji ya umati hayawezi kuimaliza Iran. Kamwe usithubutu kumtolea vitisho Muirani. Fanyia majaribio heshima kwa wengine, utapata majibu mazuri."
Msuguano baina ya Iran na Marekani ulianza mwezi Mei 2018 baada ya Rais Trump kuiondoa nchi yake katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA). Baada ya hapo Washington ilirejesha tena vikwazo dhidi ya Iran hatua ambayo inaendelea kulaaniwa kimataifa. Marekani sasa imeanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran kwa kutuma meli zake za kivita katika eneo.