Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds yafanyika katika Iran ya Kiislamu
Maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds yamefanyika kote katika Iran ya Kiislamu hii leo tarehe 31 Mei 2019 Miladia sawa na Ramadhani 25 mwaka 1440 Hijria ambapo wananchi wa matabaka mbalimbali wameonyesha hasira zao dhidi ya jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina.
Wananchi wa Iran katika maandamano ya leo Siku ya Kimataifa ya Quds wametangaza kuunga mkono kukombolewa Quds Tukufu ambapo sambamba na kupiga nara za mauti kwa Marekani, mauti kwa Israel na mauti mwa "Mabeberu wa Dunia na "Uzayuni wa Kimataifa" kwa mara nyingine wamedhihirisha chuki na hasira zao kwa jinai zinazofanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni unaouwa watoto. Wafanya maandamano hao wamesisitiza kuwa wataendelea kuonyesha kuwa Quds ni kadhia ya kwanza inayopewa kipaumbele na ulimwengu wa Kiislamu.
Waislamu duniani kote pia leo Ijumaa wameonyesha uungaji mkono wao kwa ubunifu uliofanywa na Imam Khomeini M.A Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyetangaza kuwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni Siku ya Kimataifa ya Quds. Waislamu hao wamefanya maandamano katika pembe mbalimbali za dunia na kubainisha hasira zao kwa siasa za kibaguzi zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.
Azimio la kulaani jinai za utawala wa Kizayuni, mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" na kufanyika mkutano wa Kiuchumi huko Bahrain kwa lengo la kuhuisha uhusiano kati ya baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni limetolewa na kusomwa rasmi mwishoni mwa maandamano hayo.