Viongozi wa Iran wahimiza kuungwa mkono malengo matukufu ya taifa la Palestina
Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamehimiza mno suala la kuungwa mkono malengo matakatifu ya taifa la Palestina sambamba na Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo imeadhimishwa leo na mamilioni ya wapenda haki kote ulimwenguni.
Rais Hassan Rouhani ameshiriki katika maandamano ya mamilioni ya watu mjini Tehran kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds na kusema kuwa siku hiyo ni muhimu sana katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema, hiyo ni siku ya mapambano baina ya Waislamu na mabeberu na wavamizi wote. Aidha amesema, mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" itakuwa ni nembo ya kufeli kikarne mabeberu na kamwe mpango huo hautofanikiwa.
Kwa upande wake, Ayatullah Ahmad Jannati, Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu (wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) amesema kwenye maandamano hayo kwamba, ujumbe wa maandamano ya leo ya Siku ya Kimataifa ya Quds ni mauti kwa Marekani, mauti kwa Isrel na pigo la mwisho kwa ubeberu wa Marekani.
Ayatullah Sayyid Ibrahim Raisi, Mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Iran (ambacho ni moja ya mihimili mikuu mitatu ya utawala nchini Iran) amesema kuwa, suala ka kuikomboa Quds ni la ulimwengu mzima wa Kiislamu na kwamba suala hilo ni nembo muhimu ya kusimama kidete katika kukabiliana na waistikbari na madhalimu.
Kwa upande wake Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kwenye maandamano hayo kwamba, kuwepo Wamarekani katika eneo hili nyeti kwa ajili ya kuwakandamiza Waislamu ndiko kulikozidi kutia nguvu muqawama wa watu wa eneo hili.
Mwito wa kulindwa malengo matakatifu ya Palestina umetolewa pia na viongozi wengine wengi wa Iran akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Mohammad Javad Zarif, Makamu wa Kwanza wa Rais, Es'haq Jahangiri, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah), Brigedia Jenerali Ali Fadavi, n.k.