Iran yafungua kituo kikubwa zaidi cha kutengeneza dawa Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54207-iran_yafungua_kituo_kikubwa_zaidi_cha_kutengeneza_dawa_asia_magharibi
Kituo kikubwa zaidi cha kutengeneza dawa Asia Magharibi kimefunguliwa Jumanne katika mkoa wa Alborz magharibi mwa Tehran sambamba na kuzinduliwa dawa mpya katika kituo hicho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 18, 2019 22:12 UTC
  • Iran yafungua kituo kikubwa zaidi cha kutengeneza dawa Asia Magharibi

Kituo kikubwa zaidi cha kutengeneza dawa Asia Magharibi kimefunguliwa Jumanne katika mkoa wa Alborz magharibi mwa Tehran sambamba na kuzinduliwa dawa mpya katika kituo hicho.

Kwa mujibu wa taarifa, Waziri wa Afya wa Iran Daktari Said Namaki ameshiriki katika sherehe za ufunguzi wa kituo hicho na kusema hivi sasa Iran imefanikiwa kujizalishia ndani ya nchi asilimia 97 ya dawa zote inazohitaji.

Kituo hicho cha kutengeneza dawa kinamilikiwa na shirika la Barakat Pharmaceutical na kiko katika eneo lenye ukubwa wa ekari 200.

Katika sherehe hiyo kumezinduliwa pia dawa tisa katika kituo hicho ambazo ni pamoja na Sertraline hydrochloride ya kutibu msongo wa mawazo, hydrochloride Dapoxetine ya kutibu ugumba wa wanaume, Ticagrelor ya kutibu mgando wa damu na Fusidate Sodium ya kutibu maambukizi ya damu.

Waziri wa Afya wa Iran Daktari Said Namaki

Aidha dawa zingine ambazo zimezinduliwa katika sherehe hizo ni Osteoarthritis ya kutibu maumivu ya viungo vya mifupa na recolor cell na renuderm cell za kutibu vitiligo ambao ni ugonjwa unaoathiri ngozi. Hali kadhalika katika ufunguzi wa kiwanda hicho kumezinduliwa dawa ya Vinorelbina ya kutibu saratani ya matiti na Edaravon ya kutibu wale wanaougua kiharusi.