Zarif: Iran haitasita katika kujilinda na kulihami taifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Iran haitaki mivutano lakini kama itashambuliwa, basi haitasita hata kidogo kujibu mapigo na kujihami.
Dk Mohammad Javad Zarif ambaye ameelekea nchini Marekani kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha kila mwaka cha viongozi wa ngazi za juu wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ameiambia televisheni ya NBC kwamba, mashinikizo na vitisho vya Marekani vinavyotolewa kwa visingizio mbalimbali haviwezi kuzaa matunda na kuongeza kuwa: Iwapo Marekani itafanya upambavu na kuishambulia Iran, Jamhuri ya Kiislamu itajilinda na kujitetea kwa nguvu zake zote.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Marekani imejikosesha soko kubwa la Iran katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita kutokana na vikwazo na mashinikizo yake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Dakta Zarif amesema chaguo la Tehran ni mapambano na kusimama kidete mbele ya mashinikizo ya aina zote lakini kama Marekani inatafuta njia ya kujiondoa katika hali ya sasa kwa heshima basi njia hiyo ipo.
Baada ya New York, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anatazamiwa kuekea Venezuela ambako atashiriki katika mkutano wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM). Vilevile atazitembelea nchi za Nicaragua na Bolivia.