Mousavi: Iran inaunga mkono Yemen iliyoungana
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria matukio ya hivi karibuni ya kusini mwa Yemen na kusema: "Iran imekuwa ikiunga mkono 'Yemen moja iliyoungana' na kulinda umoja wa nchi hiyo ni jukumu la Wayemeni wote."
Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo Jumatano ya jana na kuongeza kuwa muungano vamizi unaoshambulia Yemen chini ya uongozi wa Saudia na Imarati pamoja na mamluki wao, unatumia silaha za kisasa kuuawa raia na kuharibu miundo msingi ya nchi hiyo lakini pamoja na hayo wavamizi hao hawajaweza kuvunja irada na azma ya watu wa Yemen. Amesema hivi sasa njama inayotekelezwa na wavamizi hao ni ya kutaka kuigawa nchi hiyo vipande vipande.
Mousavi ameashiria moyo ya kijihadi na kusimama kidete kwa watu wa Yemen mbele ya wavamizi Wasaudi na Waimarati na kuelezea matumaini kuwa, kwa kusitisha uvamizi wa Saudia na Imarati nchini Yemen, makundi na vyama vya nchi hiyo vitaweza kufanya mazungumzo baina yao na kuhitimisha matatizo ili hatimaye iundwe serikali inayojumuisha makundi na vyama vyote.

Katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa mapigano makali baina ya makundi hasimu yanayopigana kwa niaba ya Imarati na Saudia katika mji wa Aden ambapo makumi ya wapiganaji na raia wasio na hatia wameuawa na wengine kujeruhiwa.