Salami: Usalama Ghuba ya Uajemi utapatikana kwa ushiriki wa Iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema: "Usalama katika Ghuba ya Uajemi utapatikana kwa uwepo wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo pembizoni mwa mkutano wa kila mwaka wa Wahadhiri Mabasiji wa Vyuo vya Mash'had kaskazini mashariki mwa Iran. Ameongeza kuwa: "Maadui hawataweza kuvuruga usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi.
Meja Jenerali Salami amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu haitasitisha majaribio ya aina mbalimbali ya mifumo ya kujihami na kistratijia na itendeleza mkakati wake wa kuimarisha uwezo wake wa kujihami na kumzuia adui."

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebaini kuwa, adui sasa analenga kuwawekea wananchi mashinikizo lakini taifa la Iran, kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, litaendelea kuwa na subira ya kimapinduzi na litaunga mkono Mfumo na kumtii Kiongozi Muadhamu sambamba na kujitokeza katika medani na hivyo kutoa jibu ambalo litamkatisha tamaa adui.
Meja Jenerali Salami ameendelea kusema kuwa, wananchi ni nguzo ya kimsingi ya muqawama wa Mapinduzi ya Kiislamu mkabala wa adui na leo hii wana nafasi muhimu zaidi ya wakati wowote ule.