Rais Rouhani: Iran itatekeleza awamu ya tatu ya kupunguza uwajibikaji katika JCPOA
(last modified Wed, 04 Sep 2019 13:11:33 GMT )
Sep 04, 2019 13:11 UTC
  • Rais Rouhani: Iran itatekeleza awamu ya tatu ya kupunguza uwajibikaji katika JCPOA

Rais Hassan Rouhani amesema, mazungumzo na nchi za Ulaya bado hayajafikia mwafaka kamili; na kwa msingi huo Iran itachukua hatua ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wa kutekeleza majukumu yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri. Amedokeza kuwa, mwenendo wa mazungumzo na pande shiriki katika JCPOA unapiga hatua, lakini akabainisha kwamba, pamoja na hayo ni baidi kuwa ifikapo kesho Alkhamisi mwafaka rasmi na pande hizo utakuwa umefikiwa; kwa hivyo awamu ya tatu ya kupunguza utekelezwaji wa ahadi za Iran katika JCPOA itatangazwa baina ya leo na kesho.

Rais Rouhani amesema, subira ya kistratejia na hatua ya Iran ya kukabiliana na uamuzi wa Marekani wa kujitoa katika JCPOA vimefanyika kwa umakini kamili na akasisitiza kwamba: Hatua ya tatu ya kupunguza utekelezaji majukumu ya Iran ina umuhimu mkubwa mno na ndio hatua muhimu zaidi itakayochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameongeza kuwa, kwa agizo na amri itakayotolewa, Shirika la Nishati ya Atomiki litaweza kufikia malengo yake kwa kasi kubwa mno.

Rais wa Iran amefafanua kuwa, pamoja na kuchukua hatua ya tatu, Tehran itatoa muhula mwengine wa miezi miwili kwa pande shiriki katika JCPOA; na endapo utafikiwa mwafaka, ingaliko njia ya mantiki, mazungumzo na kufikiwa makubaliano baina ya pande mbili.

Dakta Rouhani aidha amewataja viongozi wenye mitazamo ya kufurutu mpaka katika serikali ya Marekani, utawala wa ubaguzi wa rangi wa Kizayuni na baadhi ya viongozi wenye fikra mgando katika eneo kuwa ni magenge matatu ambayo hayataki kuona uhusiano sahihi na wa kiadilifu unakuwepo baina ya Iran na Marekani; na akabainisha kuwa, kudhibitiwa Ikulu ya White House na magenge hayo matatu ndio sababu ya kujitoa Marekani katika JCPOA.

Tarehe 8 Mei mwaka huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisitisha utekelezaji wa baadhi ya majkumu yake katika makubaliano ya nyuklia kulingana na kifungu cha 26 na 36 vya makubaliano hayo. Mnamo tarehe 7 Julai, Iran ilianzisha pia mchakato wa kuvuka kiwango cha asilimia 3.67 cha urutubishaji madini ya urani katika shughuli zake za nyuklia.

Halikadhalika Tehran imetangaza kwamba, endapo upande wa Ulaya utaendelea kuzembea kutekeleza majukumu yake, ifikapo tarehe 6 Septemba itaanza kutekeleza awamu ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA.../ 

Tags