JCPOA katika barabara ya upande mmoja ya Iran kupunguza uwajibikaji wake
Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema: "Mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) si barabara ya upande mmoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua maamuzi yanayofaa wakati utakapowadia."
Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran aliyasema hayo Jumapili mjini Tehran wakati alipofanya mazungumzo na Cornel Feruta, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) ambapo amekosoa utendaji wa nchi za Ulaya kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran na kusema: "Nchi za Ulaya hazijaweza kutekeleza ahadi zao katika mapatano ya JCPOA baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo."
Mapatano ya JCPOA yalifikiwa mwaka 2015 baada ya mazungumzo ya muda mrefu na yalikuwa mapatano ya pande kadhaa na pande zote hizo zilipaswa kuyatekeleza kikamilifu.
Nia njema ya Iran ilifanikisha mazungumzo ya nyuklia na kupelekea kupatikana muafaka lakini la kusikitisha ni kuwa, Marekani ilikiuka ahadi zake na ikaamua kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa.
Baada ya Marekani kukiuka sheria na kujiondoa katika mapatano ya JCPOA mwezi Mei mwaka 2018, nchi za Ulaya nazo zimeshindwa kutekeleza ahadi zao katika JCPOA na kwa msingi huo leo mapatano hayo yamebadilika na kuwa barabara ya upande mmoja.
Utekelezaji wa majukumu na ahadi katika JCPOA unahusu pande zote ambazo zilifikia mapatano hayo, yaani madola matano makubwa ambayo ni wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Iran. Kwa hivyo ni wazi kuwa pande zote zinapaswa kutekeleza ahadi na majukumu yao katika JCPOA. Kama ambavyo Iran ilionyesha nia njama katika mchakato mzima wa mazungumo na kufanikisha kufikiwa muafaka wa JCPOA, Iran pia imeendelea kuonyesha nia njema na kutekeleza ahadi zake hata baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo. Katika fremu hiyo ya kuonyesha nia njema, Iran iliamua kusibiri kwa muda wa mwaka mmoja kuona iwapo nchi za Ulaya zingetekeleza ahadi zao katika JCPOA.
Lakini baada ya kupita mwaka mmoja tokea Marekani ijiondoe katika JCPOA yaani tarehe 8 Mei 2019, na kushindwa nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao katika mapatano hayo, Iran imelazimika kuchukua hatua za kukabiliana na hali hiyo.
Katika fremu ya mapatano ya JCPOA, na kwa mujibu wa vipengee vya 26 na 36 vya mapatano hayo, Iran ilianza kupunguza utekelezaji wa ahadi zake katika JCPOA na hadi sasa imechukua hatua tatu katika kadhia hiyo.
Hatua ya tatu ya Iran katika kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya JCPOA ilichukuliwa Septemba 6 2019, na katika fremu hiyo imeweka kando vizingiti kadhaa katika uga wa utafiti na ustawi wa miradi yake ya nyuklia kwa malengo ya amani.
Tayari Iran imeshamfahamisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kuhusu hatua hiyo ya tatu alipokuwa safarini hapa Tehran. Hatua itakayoafuata ya Iran itategemea utendaji wa nchi za Ulaya, yaani Ujerumani, Ufaransa na Uingereza katika utekelezaji wa ahadi zao za JCPOA.
Nchi za Ulaya zimeanzisha mchezo wa kisiasa katika radiamali yao kuhusu hatua ya tatu ya Iran ya kupunguza uwajibaki wake katika JCPOA. Nchi hizo zimetoa madai ya kushangaza kuwa maadamu Iran inafungamana na JCPOA nazo pia zitafungamana na mapatano hayo.
Kilicho wazi ni kuwa, nchi za Ulaya zimeshindwa kabisa kutekeleza ahadi zao katika JCPOA baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa. Hali kama hiyo si ya kuridhisha kwa Iran na ujumbe wa hatua tatu ambazo Tehran imezichukua hadi sasa ni onyo kali kwa nchi za Ulaya kuwa, JCPOA ni mapatano ya pande kadhaa.
Iran imechukua hatua zilizoratibiwa katika kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya JCPOA na wakati wowote ule ambao nchi za Ulaya zitakapotekeleza ahadi zao katika JCPOA kwa maslahi ya Iran, hakuna shaka kuwa Iran itarejea tena katika utekelezaji wa majukumu yake yote katika JCPOA.
Behrouz Kamalvandi, Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran amebainisha wazi kuwa Iran inachukua maamuzi kwa mujibu wa maslahi yake ya kitaifa na kuongeza kuwa: "Iwapo nchi za Ulaya hazitatekeleza majukumu yao, basi kasi ya Iran kupunguza uwajibikaji wake itaongezeka."