Kermani: Marekani imekiuka mapatano ya nyuklia na Iran
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema hatua za hivi karibuni za Marekani dhidi ya Iran ni ukiukwaji wa wazi wa mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.
Ayatullah Mohammad Ali Muvahhedi Kermani akihutubu waumini katika Swala ya Ijumaa iliyosaliwa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran ameashiria hukumu ya hivi karibuni ya mahakama ya Marekani ya kuchukua kwa nguvu fedha za Iran zinazozuiwa nchini humo na kusema: "Hatua hiyo ni ishara kuwa Marekani haiheshimu wala kutekeleza ahadi zake na hivyo haipaswi kuaminiwa hata kidogo."
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria jukumu zito la Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo na madola ya Magharibi kuhusu vikwazo na amewashauri wawakilishi wa Iran katika mazungumzo wafanye kila wawezalo kuhakikisha taifa la Iran linapata haki zake.
Ayatullah Muvahhedi Kermani ameashiria kelele za nchi za Magharibi hasa Marekani kuhusu uwezo wa makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: "Marekani inapinga makombora haya ambayo ni ya kujihami tu katika hali ambayo yenyewe inamiliki makombora hatari zaidi za mauaji ya umati duniani."
Ayatullah Kermani amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitasalimu amari mbele ya mashinikio na vikwazo vya Marekani.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran ameashiria mazungumzo ya hivi karibuni ya Iran na Saudi Arabi kuhusu ibada ya Hija na kusema maafisa wa Hija Iran wahakikishe kuwa usalama wa mahujaji unadhaminiwa. Aidha Ayatullah Kermani amesema Saudi Arabia inashirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza kuwa ushirikiano huo ni kinyume cha mafundisho ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu.