JCPOA haina maana iwapo haiwafaidi na chochote wananchi wa Iran
(last modified Mon, 30 Sep 2019 02:36:58 GMT )
Sep 30, 2019 02:36 UTC
  • JCPOA haina maana iwapo haiwafaidi na chochote wananchi wa Iran

Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayana faida yoyote iwapo wananchi wa Iran hawastafidi chochote kutokana na mapatano hayo ya kimataifa.

Akizunguumza na vyombo vya habari jana Jumapili mjini Tehran, Mahmoud Vaezi amesisitiza kuwa, nchi za Ulaya zina wajibu maradufu wa kutekeleza ahadi zao na kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo, baada ya Marekani kujiondoa kwenye mapatano hayo.

Amebainisha kuwa, mashinikizo na vikwazo vya kiuchumi vya Marekani vilikusudia kuifanya Iran itengwe na jamii ya kimataifa, lakini ndoto hiyo haijaweza kufua dafu.

Kauli ya Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Iran ni radiamali kwa vitisho vya nchi za Ulaya ambazo zimedai kuwa zitajiondoa kwenye makubaliano hayo ya nyuklia iwapo Iran eti haitafungamana kikamilifu na mapatano hayo.

Viongozi wa nchi za EU wamesema iwapo Iran itachukua hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake kwenye makubaliano hayo mwezi Novemba mwaka huu, basi nchi hizo za Ulaya zitaanza kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.

Rais Donald Trump anazishinikiza nchi za Ulaya zifuate mkondo wa US na kujiondoa JCPOA

Kutokana na EU kutofungamana kikamilifu na mapatano hayo kwa mashinikizo ya Marekani, Septemba 6 Tehran ilianza kutekeleza hatua ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia ya JCPOA, na hatua ya nne inatazamiwa kuanza kutekelezwa mwezi Novemba.

Mwezi Mei mwaka jana, Rais Donald Trump alichukua hatua ya upande mmoja na kuiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya kimataifa yenye baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Tags