Rouhani: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni ugaidi wa kiuchumi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56639-rouhani_vikwazo_vya_marekani_dhidi_ya_iran_ni_ugaidi_wa_kiuchumi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA ni fedheha kwa Marekani na kuongeza kuwa: "Fedheha kubwa zaidi kwa Marekani ni kuwawekea watu wa Iran vikwazo vya dawa na chakula."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2019 09:40 UTC
  • Rouhani: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni ugaidi wa kiuchumi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA ni fedheha kwa Marekani na kuongeza kuwa: "Fedheha kubwa zaidi kwa Marekani ni kuwawekea watu wa Iran vikwazo vya dawa na chakula."

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran katika Kikao cha 66 cha Shirika la Afya Duniani cha Mawaziri wa Afya wa Nchi za Eneo la Mediterania Mashariki na kusisitiza kuwa; "Marekani imetekeleza jinai dhidi ya binadamu na hatua inazochukua ni ugaidi wa kiuchumi." Rais wa Iran ameongeza kuwa: "Wasomi, watafiti, wajasiriamali na wanaviwanda Wairani wanaielekeza nchi katika kujitosheleza kikamilifu licha ya kuwepo mashinikizo yasiyo na kifani ya kiuchumi na vikwazo vya kidhalimu."

Rais Rouhani amesisitiza kuwa, Wairani milioni 83 hawatasahau jinai za Marekani na kuongeza kuwa Marekani ndiyo itakayoshindwa huku Iran ikipata ushindi katika nyuga za maadili mema, ubinadamu na siasa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kubaini kuwa, vita na ugaidi ni sababu kuu zinazovuruga afya ya jamii na kuongeza kuwa, kuvamiwa kijeshi na kukaliwa kwa mabavu Yemen, Syria, Iraq na Afghanistan kuna maana kuwa, watu wa nchi hizo wanakumbwa na matatizo makubwa ya kiafya.

Rais Rouhani amesema Iran haiwasahau majirani zake wanaokumbwa na masaibu na kuongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa bega kwa bega na watu wa Iraq na Syria katika kuwapa huduma za afya."

Aidha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu iko pamoja na watu wanaodhulumiwa wa Palestina katika mapambano yao dhidi ya uvamizi na unyama wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Rais Rouhani ameendelea kusema kuwa, Iran itaendelea kuwatumia dawa na chakula watu wa Yemen na ina fakhari kutokana na kazi yake hiyo.