Zarif ataka kusitishwa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mwito wa kusitishwa uvamizi na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria.
Mohammad Javad Zarif ametoa mwito huo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kusisitiza kuwa, mgogoro wa Syria unapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa njia za diplomasia na mazugumzo.
Ingawaje hakutaja moja kwa moja operesheni ya kijeshi ya Uturuki kaskazini mwa Syria kwenye ujumbe wake huo, lakini mwanadiplomasia huyo wa Iran amebainisha kuwa, ni muhimu kutenganishwa kati ya raia na wapiganaji, ili kuzuia umwagaji damu wa raia wasio na hatia.
Mapema jana Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilieleza juu ya wasiwasi wake kuhusu operesheni ya kijeshi ya Uturuki dhidi ya Syria na kusisitiza kuwa, kutokana na hali mbaya ya kibinadamu na kuwa hatarini maisha ya raia, kuna udharura jeshi la Syria lisitishe operesheni zake za kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Kadhalika taarifa iliyotolewa jana na wabunge wa Iran ilikosoa kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya mashambulizi yanayoendelea kufanywa na jeshi la Uturuki huko kaskazini mwa Syria na kusema: Kimya cha nchi zinazodai kutetea haki za binadamu na Umoja wa Mataifa mbele ya mashambulizi hayo kitasajiliwa katika historia.
Jumatano iliyopita Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki aliliamuru jeshi la nchi hiyo kufanya mashambulizi dhidi ya eneo la kaskazini mwa Syria kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi na kuwaangamiza wanamgambo wa Kikurdi katika mpaka wa nchi hizo mbili ambao Ankara inasema wanashirikiana na kundi la wapiganaji wa PKK wanaotaka kujitenga maeneo ya Wakurdi nchini Uturuki.