"Iran haitakuwa mtekelezaji pekee wa makubaliano ya nyuklia"
Naibu Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Tehran haipaswi kuwa mtekelezaji pekee wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA iwapo upande wa pili hautatekeleza wajibu wake.
Es'hagh Al Habib alisema hayo jana Alkhamisi katika kikao cha wazi cha Kamati ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa na kufafanua kuwa, "Marekani sio tu ilichukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa kwenye makubaliano ya JCPOA kinyume cha sheria za kimataifa, lakini pia imeendelea kuzitishia nchi nyingine ambazo zinafungamana na mapatano hayo."
Ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuchukua hatua za kupunguza uwajibikaji wake kwenye makubaliano hayo iwapo nchi zilizosalia kwenye JCPOA hazitachukua hatua madhubuti zenye maslahi kwa Iran.
Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, hatua ya Marekani ya kukiuka mapatano mbalimbali ya kimataifa inadhalilisha na kufanya kuwa dhaifu taasisi za kimataifa.
Tehran imesitisha kisheria utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo kwa mujibu wa vipengee nambari 26 na 36 vya JCPOA, ikiwa ni jibu kwa nchi za Ulaya ambazo zimeshindwa kuchukua hatua za kivitendo ili kuyanusuru mapatano hayo.