Rouhani: Juhudi za Marekani za kutaka Iran itengwe zimefeli
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56825-rouhani_juhudi_za_marekani_za_kutaka_iran_itengwe_zimefeli
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Marekani imefeli katika jitihada zake za kutaka kutoa pigo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kuifanya itengwe katika uga wa kimataifa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 24, 2019 13:06 UTC
  • Rouhani: Juhudi za Marekani za kutaka Iran itengwe zimefeli

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Marekani imefeli katika jitihada zake za kutaka kutoa pigo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kuifanya itengwe katika uga wa kimataifa.

Rais Rouhani amesema hayo mapema leo kabla ya kuelekea Baku, mji mkuu wa Azerbaijan alikoenda kushiriki mkutano wa 18 wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) ambapo ameeleza bayana kuwa, "Iran haitosalimu amri kwa matakwa ya wasioitakia mema na kuitaka isishiriki kikamilifu katika shughuli za mfumo wa kimataifa."

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, Wamarekani tangu hapo mwanzo wamekuwa wakifanya juu chini kuona Jamhuri ya Kiislamu inatengwa na kuachwa peke yake, lakini kwa Rehema za Allah nafasi ya Iran miongoni mwa mataifa ya dunia imekuwa ikiimarika siku baada ya siku.

Amesema njama za maadui ukiwemo ugaidi wa kiuchumi uliopewa jina la mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ya Marekani zimeshindwa kuipigisha magoti Iran ya Kiislamu na badala yake taifa hili limegeuka kuwa muhimu na lenye ushawishi mkubwa kieneo na kimataifa.

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika kikao cha mawaziri wa nchi za jumuiya ya NAM

Rais Hassan Rouhani amebainisha kuwa, sera ghalati za utawala wa Donald Trump zimepelekea kutengwa zaidi Marekani katika uga wa kimataifa.

Tayari Dakta Rouhani amewasili Baku kushiriki mkutano huo wa 18 wa marais na viongozi wa nchi 120 wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) unaoanza kesho Oktoba 25 hadi 26.