IRGC: Uvamizi wowote dhidi ya Iran utakabiliwa na jibu kali
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema jaribio lolote la maadui la kujaribu kuvamia ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran litapokea jibu kali.
Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa IRGC ameyasema hayo leo Alkhamisi katika ufunguzi wa miradi ya maendeleo katika mkoa wa Alborz ulioko kaskazini mwa nchi na kusisitiza kuwa, "Iran imewazika maadui katika kaburi la ndoto zao."
Amefafanua kuwa, mbali na Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Saudi Arabia na Uingereza, adui mwingine mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ni umaskini na uchochole.
Meja Jenerali Hussein Salami ameeleza bayana kuwa, njama za maadui za kuusambaratisha Mfumo wa Kiislamu hapa nchini hii leo zimevurugika kwa kiasi kikubwa kuliko wakati mwingine wowote ule.
Kamanda Mkuu wa SEPAH amebainisha kuwa, licha ya vikwazo na mashinikizo ya maadui, lakini Jamhuri ya Kiislamu imeendelea kukwea na kufika katika upeo wa juu kwenye sekta ya sayansi na teknolojia.
Ameongeza kuwa, uwezo mkubwa wa jeshi la Iran hauwezi kupenyeka wala kushindika na kwamba: "Kwa uwezo wa Allah, tutaendelea kulinda mipaka na kila shibri ya ardhi ya taifa hili, sambamba na uhuru wake wa kujitawala na mipaka."