Tehran: Nchi zilizozaa ugaidi zisiibebeshe Iran matatizo yao
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu matamshi ya kipuuzi na yasiyo na msingi yaliyotolewa na baadhi ya washiriki wa kikao kilichopewa jina la "Mazungumzo ya Manama" huko Bahran na kusisitiza kuwa tuhuma zilizotolewa na watu hao dhidi ya Iran hazina msingi.
Mkutano wa 15 wa Usalama wa Kieneo uliopachikwa jina la "Mazungumzo ya Manama" ulianza juzi Ijumaa katika mji mkuu huo wa Bahrain.
Adel al Jubair, Waziri Mshauri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia na Anwar Gargash, Waziri Mshauri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) jana Jumamosi waliituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa eti inafanya vitendo vya uharibifu kwenye eneo hili.
Hata hivyo Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran leo Jumapili amejibu tuhuma hizo zisizo na mashiko akisema: Nchi ambazo zenyewe ndizo wazalishaji na waenezaji wa ugaidi na misimamo mikali duniani, nchi ambazo zimeshindwa hata kuchunga msingi wa ujirani mwema na zinaingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na vile vile zinahatarisha usalama wa eneo hili hasa kwa maamuzi yao ghalati ya kumimina wanajeshi wa madola ajinabi ya kibeberu hapa Mashariki ya Kati; hazina haki ya kuibebeshwa matatizo yao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Aidha amesema, uvamizi wa kijeshi nchini Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia na jinai kubwa za wavamizi hao za kuua na kujeruhi makumi ya maelefu ya wanawake, watoto wadogo na watu wengine wasio na hatia sambamba na kuangamiza miundombinu yote ya Yemen zitambue kuwa jinai zao hizo kamwe haziwezi kufutika kwenye kumbukumbu za watu wa eneo hili na duniani kiujumla.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha amezitaka nchi hizo zisijibabaishe na kujifanya hazielewi kuwa zimeshindwa vibaya huko Yemen na katika njama zao zote kwenye ulimwengu wa Kiislamu.