Zarif: Nchi za Ulaya zitekeleze majukumu yao katika mapatano ya nyuklia
(last modified Mon, 09 Dec 2019 07:53:21 GMT )
Dec 09, 2019 07:53 UTC
  • Zarif: Nchi za Ulaya zitekeleze majukumu yao katika mapatano ya nyuklia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijaridhishwa na kiwango ambacho nchi za Umoja wa Ulaya zinatekeleza mapatano ya nyuklia ya JCPOA."

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo mapema Jumatatu baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Istanbul na kusisitiza kuwa: "Kuna udharura kwa pande zote zilizoafiki mapatano ya JCPOA kuyatekeleza."

Ameongeza kuwa kadhia ya kutoridhishwa na namna nchi za Ulaya zinavyotekeleza JCPOA imewasilishwa na Iran, China na Russia kwa kamati ya mapatano hayo.

Zarif aidha ameashiria hatua ya Iran kupunguza kiwango cha utekelezaji wa ahadi zake katika mapatano ya JCPOA baada ya nchi za Ulaya kukiuka mapatano hayo na kusema: "Iwapo wengine watatekeleza kikamilifu JCPOA, Iran itasitisha hatua ilizochukua kwa mujibu wa kipengee cha 36 cha mapatano hayo."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameitaja kuwa chanya hatua ya nchi sita za Umoja wa Ulaya kujiunga na mfumo wa kifedha wa INSTEX, ambao ni maalumu kwa ajili ya mabadilishano ya kifedha ya Iran na Ulaya, na kuongeza kuwa, kuna uwezekano wa kuanza kutekelezwa mfumo huo katika mustakabali.

Zarif aidha ameashiria safari yake mjini Istanbul na kusema: "Lengo la safari nchini Uturuki ni kushiriki katika Kikao cha Nane cha Mawaziri cha 'Mchakato wa Istanbul na Moyo wa Asia' ambao lengo lake ni kuleta uthabiti, usalama na ustawi nchini Afghanistan.

Aidha amebaini kuwa, kwa kuzingatia uchaguzi wa rais nchini Afghanistan na mchakato wa amani,  kuna udharura kwa nchi za eneo na jirani kushiriki katika mkondo wa amani na ujenzi mpya wa nchi hiyo.

 

Tags