Iran: Tuko tayari kushirikiana na nchi zote za Kiislamu kutengeneza akili bandia
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kushirikiana na nchi zote za Kiislamu katika kustawisha utaalamu wa Akili Bandia (Artificial Intelligence).
Rais Hassan Rouhani ambaye yuko mjini Kuala Lumpur Malaysia kushiriki katika kikao maalumu cha viongozi wa nchi za Kiislamu, leo Jumatano ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, maendeleo ya siku za usoni ya kiuchumi duniani yatategemea sana mfumo wa dijitali na kwamba kupiga hatua za kimaendeleo katika suala hilo hakuwezekani bila ya kuwepo ushirikiano wa nchi mbalimbali.
Rais Rouhani ameitikia mwaliko wa Waziri Mkuu wa Malaysia, Mahathir Mohamad wa kushiriki kwenye kikao hicho cha viongozi wa nchi za Kiislamu cha "Kuala Lumpur 2019."
Miongoni mwa malengo ya kikao hicho cha wakuu wa nchi za Kiislamu huko Malaysia ni kutafuta njia za maana za kutatua matatizo ya kimataifa na kuboresha hali za Waislamu katika kona mbalimbali za dunia.
Kikao cha "Kuala Lumpur 2019" kimehudhuriwa na watu 400, ambapo 250 kati yao ni wakuu wa nchi, viongozi wa ngazi za juu, wasomi na wanasiasa mashuhuri kutoka nchi 52 duniani. Kikao hicho kimeanza leo Jumatano na kinatarajiwa kuendelea hadi tarehe 21 Disemba.
Siku ya Ijumaa, Rais Hassan Rouhani anatarajiwa kutembelea Japan kwa ajili ya kuonana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abe Shinzo.