Taarifa ya Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni Iran kuhusu Sheikh Zakzaky
Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni Iran limetoa taarifa likitaka wakuu wa sera za kigeni katika nchi za Kiislamu wafuatilie kadhia ya kufungwa jela kinyume cha sheria Allamah Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na kuhakikisha anatendewa haki.
Katika taarifa yake ya Alkhamisi usiku, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni Iran limesema, zaidi ya miaka minne imepita tokea kujiri jinai ya kuuawa Waislamu huko Zaria nchini Nigeria na Sheikh Zakzaky kuwekewa vizingiti visivyo vya kawaida katika masuala ya afya na tiba. Taarifa hiyo imesema, ni jambo la kusikitisha kuona kuwa, watawala wa kijeshi nchini Nigeria wameweka vizingiti dhidi ya haki zake za binadamu na sasa wamemhamisha Sheikh Zakzaky katika gereza ya Kaduna.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria yuko katika hali mbaya sana ya kiafya gerezani na anaugua magonjwa kadhaa bali yuko katika hali mahututi, jambo ambalo limezusha wasi wasi mkubwa.
Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni la Iran limekumbusha kuwa hadi sasa watoto sita wa Sheikh Zazaky wameshauawa shahidi na dada yake naye pia ameuawa shahidi. Aidha taarifa hiyo imesema kwa kuzingatia uzembe au upuuzaji uliopo katika kumpa Sheikh Zakzaky matibabu, wakuu wa Nigeria watabebe dhima kuhusu chochote kitakachotokea kuhusu mwanazuoni huyo mpigania mageuzi.
Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky, 66, na mkewe walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia na kushambulia Husainia iliyoko katika mji wa Zaria. Katika shambulio hilo, Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria wasiopungua 1,000, wakiwemo wana watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi.