Maulamaa wa Kiislamu wataka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky
Miito mbalimbali ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeendelea kutolewa na shakhsia, wanaharakati na Maulamaa wa Kiislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia.
Ayatullah Abdullah Javad-Amoli, Marjaa Taklidi wa Qum Iran sambamba na kutoa wito wa kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema kuwa, mwanazuoni huyo amejitolea pakubwa katika Uislamu wakiwemo watoto wake waliouawa shahidi katika njia ya Uislamu.
Ayatullah Javad-Amoli amesema hayo mjini Qum Iran alipokutana na mabinti wa Sheikh Zakzaky.
Kwa upande wake Ayatullah Mohsen Araki amesema katika mazungumzo yake na mabinti wa Sheikh Zakzaky kwamba, kuna haja ya kufanyika juhudi katika asasi za kimataifa kwa ajili ya kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky.
Ayatullah Nassir Makarim Shirazi mwanazuoni mwingine na Marjaa Taklidi wa mjini Qum hapa Iran yeye ameitaka serikali ya Nigeria iwajibike na ihitimishe dhulma dhidi ya Sheikh Zakzaky.
Ayatullah Sheikh Makarim Shirazi ameeleza kusikitishwa mno na kimya cha watetezi wa haki za binadamu na viongozi wa nchi za Kiislamu kuhusiana na hali anayokabiliwa nayo Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kkiislamu ya Nigeria.
Sheikh Ibrahim Zakzaky, (66) na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussaynia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.