Rouhani: Watu wa Iran ni watiifu kwa mapinduzi na kiongozi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58221-rouhani_watu_wa_iran_ni_watiifu_kwa_mapinduzi_na_kiongozi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Watu wa Iran ni watiifu kwa Mapinduzi, Kiongozi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 31, 2019 09:04 UTC
  • Rouhani: Watu wa Iran ni watiifu kwa mapinduzi na kiongozi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Watu wa Iran ni watiifu kwa Mapinduzi, Kiongozi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo Jumanne katika hafla ya kuzindua safari za treni ya umeme ya kutoka eneo la Golshahr kuelekea Hashtgerd katika mkoa wa Alborz magharibi mwa Tehran. Rais Rouhani ameashiria kujitolea muhanga wananchi kwa ajili ya Uislamu, Iran na Mapinduzi na kuongeza kuwa: "Katika siku za hivi  karibuni mamilioni ya wananchi wamejitokeza katika maandamano kwa ajili ya usalama, utulivu, kuunga mkono Mapinduzi, Kiongozi Muadhamu na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na nukta hii inaashiria utiifu wao."

Rais Rouhani ameendelea kusema kuwa,  kujitokeza mamilioni ya wananchi katika maandamano ni jambo ambalo limewakasirisha maadui.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa wananchi wa Iran wamewachagua viongozi wao kupitia upigaji kura na kwa msingi huo kuna haja ya kuwa na matumaini kuhusu mustakabali.

Rais Rouhani akizundua treni ya umeme katika mkoa wa Alborz magharibi mwa Tehran

Hali kadhalika Rais Rouhani amekumbusha kuwa katika zama za vita vya kulazimishwa (vya Iraq dhidi ya Iran) na zama za vikwazo, wananchi wa Iran wamekuwa wakijitahidi kwa ajili ya uhuru na kujitegemea na hivyo hawako tayari kuacha nchi itekwe na waporaji.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ameashiria mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Iran, Russia na China katika Bahari ya Oman na Bahari ya Hindi na kusema madola ya kibeberu na yenye kupora utajiri wa wengine yamekasirishwa mno kuona madola makubwa duniani yakifanya mazoezi ya pamoja na Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.