Rouhani: Watu wa Asia Magharibi watakabiliana na dhulma za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58799-rouhani_watu_wa_asia_magharibi_watakabiliana_na_dhulma_za_marekani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema wananchi wa nchi za eneo la Asia Magharibi watakabiliana na dhulma na ubeberu wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 28, 2020 11:51 UTC
  • Rais Hassan Rouhani
    Rais Hassan Rouhani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema wananchi wa nchi za eneo la Asia Magharibi watakabiliana na dhulma na ubeberu wa Marekani.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kaunti ya Pakdasht katika mkoa wa Tehran wakati wa uzinduzi wa kituo cha kusafisha maji na kuongeza kuwa, "Marekani ambayo imekuwa ikidai kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu na demokrasia inaendeleza harakati zake za ukandamizaji na dhulma dhidi ya watu wa kanda hii na kote duniani kwa ujumla, lakini watu wa eneo hili watapambana na dhulma hizo."

Ameashiria mashinikizo ya kiwango cha juu ya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran baada ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambapo amebainisha kuwa, licha ya vikwazo vya kidhalimu na mashinikizo hayo ya Marekani dhidi ya Iran, lakini taifa hili limesimama kidete kuhakikisha kuwa linafikia upeo wa juu wa maendeleo na kutimiza ndoto zao.

Amesema, "tunadhani nguvu na uwezo ni muhimu tu katika kusimama dhidi ya Marekani na mabeberu, hapana, nguvu ni muhimu pia katika kuamiliana na mafariki, majirani na ndugu; kwa kuwa kama huna nguvu hata nchi ndogo jirani itakunyanyasa."

Rais Rouhani akizindua Kituo cha Saba cha Kutibu Maji Tehran

Rais wa Iran ameongeza kuwa, viongozi wawili wa Ulaya walimuambia kuwa (Rais wa Marekani Donald) Trump aliwaambia kuwa Iran itasambaratika ndani ya miezi mitatu kutoka na mashinikizo ya hali ya juu, lakini taifa kubwa la Iran limeyavumilia machungu na kipindi hicho cha changamoto na kukivuka salama.

Kuhusu uchaguzi ujao wa Bunge, Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa,  anatumai wananchi wa Iran watajitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo kwa kuwa zoezi hilo linalotazamiwa kufanyika Februari 21 litakuwa na athari kwa sera za kieneo na kimataifa, na uwezo wa taifa hili.