Watu 435 walioambukuzwa Corona nchini Iran wapona
Naibu Waziri wa Afya wa Iran Dkt. Alireza Raisi amesema hadi sasa watu 435 waliombukizwa ugonjwa wa COVID-19 maarufu kama Corona wamepona na wamepewa ruhusa ya kuenda nyumbani kutoka hospitali.
Akizungumza na waandishi habari Jumanne mjini Tehran, Raisi amesema watu hao wote waliopona wako katika hali nzuri hivi sasa.
Aidha ameongeza kuwa, hadi kufikia jana adhuhuri kulikuwa na kesi mpya 835 za waliombukizwa kirusi cha Corona kote Iran na hivyo kwa ujumla walioambukizwa ni 2,336. Aidha amesema hadi kufikia sasa watu 77 wamepoteza maisha nchini kutokana na kirusi cha Corona.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, hadi sasa zaidi ya watu elfu 89 wameathirika na kirusi cha Corona kote duniani ambapo kati yao watu elfu 45 wamepona huku wengine zaidi ya 3000 wakifariki dunia. Kwa sasa wimbi la kuenea Corona duniani limezusha wasiwasi mkubwa na jamii ya madaktari nchini Iran iko mstari wa mbele kwa kufanya kazi usiku na mchana katika kupambana na kirusi hicho kinachoenea kwa kasi. Aidha wataalamu nchini Iran wako mbioni kuunda chanjo ya kirusi cha Corona aina ya COVID-19 na inatarajiwa kuwa katika siku zijazo watatangaza mafanikio katika uga huo.