Watu karibu 3,000 wamepona Corona nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59669-watu_karibu_3_000_wamepona_corona_nchini_iran
Wizara ya Afya ya Iran imetangaza kuwa hadi sasa watu 2,731 waliokuwa wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19, maarufu kama Corona, nchini Iran wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupokea matibabu hospitalini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2020 01:11 UTC
  • Watu karibu 3,000 wamepona Corona nchini Iran

Wizara ya Afya ya Iran imetangaza kuwa hadi sasa watu 2,731 waliokuwa wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19, maarufu kama Corona, nchini Iran wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupokea matibabu hospitalini.

Dk Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran akizungumza na waandishi habari Jumanne mjini Tehran amesema hadi sasa watu 8042 wameambukizwa COVID-19 nchini Iran. Aidha amebainisha masikitiko yake kuwa hadi sasa watu 291 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo nchini Iran. 

Hadi hivi sasa virusi hivyo vimeshaenea katika nchi 119 duniani huku idadi ya watu wanaoambukizwa virusi hivyo ndani ya China ikizidi kupungua siku baada ya siku. 

Dk Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran

Takwimu za hivi karibuni kabisa zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu laki moja na elfu 19 wameambukizwa virusi vya Corona katika maeneo mbalimbali ya dunia ambapo zaidi ya 66,000 kati yao wamepona huku zaidi ya elfu nne wakiaga dunia.