Mousavi: Marekani haina hadhi ya kuzungumzia masuala ya haki za binadamu
(last modified Sat, 14 Mar 2020 03:03:35 GMT )
Mar 14, 2020 03:03 UTC
  • Mousavi: Marekani haina hadhi ya kuzungumzia masuala ya haki za binadamu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini Iran na kusema kuwa, utawala wa Marekani haustahiki wala hauna hadhi ya kisiasa, kisheria na kimaadili ya kutoa maoni kuhusu masuala yanayohusiana na haki za binadamu.

Sayyid Abbas Mousavi ameashiria baadhi ya hatua haribifu za Rais wa Marekani ikiwa ni pamoja na kutoa matamshi ya kibaguzi, kutetea ubaguzi wa kidini, kutumia vibaya wanawake katika masuala ya anasa na uasherati na kuunga mkono na kuukingia kifua utawala unaoua watoto wa Israel na kusema kuwa: Utawala kama huu hauna hadhi ya kutoa maagizo kwa nchi nyingine kuhusiana na haki za binadamu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo akikiri kwamba mafundisho ya kusema uongo na ulaghai yalikuwa sehemu ya kazi zake wakati alipokuwa mkuu wa shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA na kusema: Ripoti za uongo zinazotayarishwa na Wamarekani kuhusiana na nchi nyingine ikiwemo Iran ni mbinu ya wazi inayotumiwa na Pompeo na wenzake katika shirika la CIA na kwa msingi huo ripoti hizo hazina thamani yoyote.

Abbas Mousavi

Abbas Mousavi ameeleza wasiwasi wake kuhusiana na uraibu wa viongozi wa Marekani wa kusema uongo, ubaguzi wa kupanga, sera za kupiga vita wageni, ukatili na kutumia mabavu, na kusema siasa za kinyama na zisizo za kibinadamu dhidi ya wahajiri za watawala wa Marekani ndio mfano mbaya zaidi wa ubaguzi, na kwamba hatua ya serikali ya Washington ya kutenganisha baina watoto wadogo wa wahajiri na wazazi wao kwa ajili ya kuwatia woga na wahka wahamiaji hao ni mwenendo wa kutia aibu zaidi wa serikali ya nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani dhidi ya Iran inakamilisha propaganda chafu za taasisi tegemezi kwa Marekani kama Amnesty International ambayo inatekeleza kivitendo siasa na sera za serikali ya Washington chini ya mwavuli wa taasisi isiyo ya kiserikali.